📌RHODA SIMBA
WITO umetolewa kwa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, kutoa mafunzo kwa wanachama wa klabu za waandishi wa Habari katika mikoa, ili kuimarisha weledi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na usambazaji wa Habari kwa umma.
Wito huo umetolewa leo, Januari 28,2025 Mkoani Singida na Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wanachama wa klabu za waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kuhusu matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na tafiti nyingine za Takwimu yaliyoandaliwa na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Kufanya hivyo kutaongeza kutangazwa kwa shughuli nyingi zaidi za maendeleo zinazofanyika mikoani zikiwemo zinazofanywa na wananchi wenyewe kama kilimo, ufugaji, uvuvi na nyinginezo nyingi ambazo zinagusa maisha ya siku ya wananchi sio tu wa vijijini bali hata wanaoishi mijini,
Dendego amesema kuwa, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na Mpango Kabambe wa Pili wa Maendeleo ya Takwimu nchini (TSMP II).
Aidha amesema kuwa Mafunzo hayo yanakwenda sambamba lengo kuu la Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 ambalo ni kuongeza uelewa, uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Serikali, wananchi na wadau wote ili kupanga mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na mazingira.
Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda, amesema kuwa kwa sasa serikali ipo katika Awamu ya Tatu na ya mwisho ya utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi.
Awamu hiyo inajumuisha uchakataji, uchambuzi na uandishi wa ripoti pamoja na usambazaji, kufanya mafunzo na kuhamasisha matumizi ya matokeo ya Sensa.
Ameeleza kuwa awamu hiyo ni tofauti na tafiti nyingine za kitakwimu ambazo matokeo yake hutolewa mara moja kwa mkupuo, matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi hutolewa hatua kwa hatua kufuatana na Kalenda ya Utoaji wa Matokeo.
Kama mlivyoona wakati wa zoezi la kuhesabu watu, Dodoso la Sensa lilikuwa na maswali karibu ya 100, hivyo taarifa zilizokusanywa zilikuwa nyingi kwa maana hiyo uchambuzi wake hufanyika hatua kwa hatua hadi kupata matokeo na kutoa ripoti kamili.
0 Comments