📌BAHATI MSANJILA
Wafanyabiashara wa Jiji
la Dar es Salaam wamehimizwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika Pori
la Akiba Pande, ambalo linatarajiwa kuwa kivutio kikubwa cha utalii
nchini.
Hii
ni baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
(TAWA) kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya miundombinu ya michezo ya watoto,
huduma za malazi, na vivutio vya kitalii vyenye viwango vya kimataifa.
Wito
huu umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula
(Mb), alipokuwa akijibu swali la Mhe. Mariam Nassoro Kisangi (Mb) Bungeni
jijini Dodoma, akizungumzia hatua za serikali katika kuendeleza Pori la Pande
kama kivutio cha utalii.
Mhe.
Kitandula amefafanua kuwa tangu mwaka wa fedha 2021/2022, Wizara ilianzisha
miradi mikubwa ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na maeneo ya kupumzikia wageni
(Picnic Sites) na kambi za watalii (Public Camp Sites).
Aidha,
mwaka 2023/2024 Wizara ilianzisha bustani ya wanyamapori na kuongeza idadi ya
wanyama katika pori hilo, ambapo kwa sasa kuna zaidi ya 100 ya aina mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na duma, simba, mamba, pundamilia, na swala granti.
Pori
la Akiba Pande limeboreshwa kwa miundombinu ya barabara inayopitika mwaka
mzima, huku lango kuu la kuingilia likiwa limejengwa ili kuboresha huduma kwa
watalii.
Kwa
juhudi hizi, idadi ya watalii wanaotembelea eneo hilo imeongezeka kwa kiasi
kikubwa, ambapo tangu mwaka 2023 hadi 2024, watalii 4,606 walitembelea pori
hilo.
Fursa
hizi za uwekezaji katika Pori la Pande zinatoa mwanya kwa wafanyabiashara na
wawekezaji kujiunga na juhudi za serikali za kuendeleza sekta ya utalii na
kuboresha miundombinu ya huduma za kitalii, huku pia ikichangia katika ukuaji
wa uchumi wa jiji la Dar es Salaam na taifa kwa ujumla.
0 Comments