BENKI ya NMB imekuwa
taasisi ya kwanza ya kifedha Afrika Mashariki kutwaa tuzo ya Mwajiri kinara,
Inayotolewa na taasisi ya kimataifa ya TOP EMPLOYER, na hivyo kuwa miongoni mwa
taasisi 2400 duniani ambazo zimefanikiwa kupata tuzo hiyo.
Akiongea na waandishi wa
habari wakati wa kutambulisha tuzo hiyo Afisa Mkuu rasilimali watu wa benki ya
NMB Emmanuel Akonaay, amesema kigezo kikubwa kinachoangaliwa kwenye upataji wa
tuzo hiyo ya kimataifa ya TOP EMPLOYER ni ustawi wa wafanyakazi wakiangalia
zaidi utendaji kazi, mifumo na sera za taasisi husika upande wa rasilimali watu
kama vinakidhi viwango vya kimataifa.
Bwana Akonaay amevitaja
vigezo sita vinavyozingatiwa ili taasisi iweze kupata tuzo hiyo ya kimataifa ya
TOP EMPLOYER , ambavyo ni mikakati ya taasisi husika kwa wafanyakazi wake,
mchakato mzima unaotumika kwenye taasisi katika kuwapata wafanyakazi bora na
uendelezaji wa wafanyakazi kwenye taasisi husika.
Vigezo vingine ni namna
bora ya kuwatumia wafanyazi kulingana na uwezo na vipaji vyao kwa matokeo
chanya ndani ya taasisi pamoja na usawa wa kijinsia kwa wafanyakazi na viongozi
kwenye taasisi husika.
NMB kupata tuzo ya
kimataifa ya TOP EMPLOYER inaifanya benki hiyo kuwa taasisi ya kwanza ya kifedha
Afrika Mashariki kupata Tuzo hiyo, hivyo inakuwa miongoni mwa taasisi 2400
duniani ambazo zimefanikiwa kupata tuzo hiyo ambazo kwa ujumla wake zimeajiri
wafanyakazi million 13.
Katika kudhihirisha benki
ya NMB ni mwajiri bora, mwaka 2022 benki hiyo ilitambuliwa na chama cha waajiri
Tanzania (ATE) kuwa mwajiri bora wa mwaka , mwaka 2023 benki ya NMB ilitangazwa
na ATE kushika nafasi ya pili ya mwajiri bora na mwaka huo huo benki ya NMB
ilitambuliwa kitaifa na kimataifa kuwa ni taasisi inayozingatia usawa wa
kijinsia kwa wafanyakazi wa kawaida na utawala.
0 Comments