WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Ridhiwani
Kikwete amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri nchini kusimamia mapato ili
kulipa mishahara na malimbikizo ya madai kwa watumishi ikiwemo fedha za likizo.
Kadhalika
amewataka wakurugenzi kulipa posho za watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo
watendaji wa Kata.
Kikwete
ameyasema hayo leo Januari 15,2025 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha 30
cha Baraza kuu la Chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU)
Amesema
Serikali haitawafumbia macho waajiri ambao hawatekelezi takwa la kisheria
ikiwemo kuhuisha mabaraza ya wafanyakazi, na kwamba Serikali imesikia na
kuelewa changamoto zote zilizoanishwa na ipo tayari kufanyia kazi.
Awali
akisoma Risala Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU)
Katibu wa Chama hicho Rashid Mtima, amebainisha changamoto mbalimbali
wanazokutana nazo watumishi wa umma ikiwemo fedha za likizo kutolipwa kwa
wakati, Malipo ya Leseni kwa Kada ya Afya,Fedha za Uhamisho Kutolipwa, pamoja
na Changamoto za Mfumo wa PEPMIS.
Akizungumzia
kuhusu mfumo wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma (PEPMIS) Mtima
amesema umekumbwa na changamoto za mtandao na ukosefu wa mafunzo kwa watumishi
waliopo maeneo ya vijijini, hali inayozuia utekelezaji bora wa mfumo huo.
Pia,
Mtima alikumbusha kuwa baadhi ya halmashauri hazijahuisha mabaraza ya
wafanyakazi kama inavyotakiwa kisheria. Hadi sasa, Halmashauri 41 kati ya 185
hazijafanya hivyo, jambo linalozuia utatuzi wa changamoto za watumishi kwa
wakati.
Hata
hivyo, TALGWU ilipongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan katika kuboresha utumishi wa umma. Miongoni mwa hatua
zilizotajwa ni pamoja na kupandisha madaraja ya watumishi, kuboresha mifumo ya
kikokotoo cha mafao, na kuimarisha miundombinu ya usafiri, ikiwa ni pamoja na
utekelezaji wa mradi wa treni ya umeme (SGR).
Kikao
hicho kimehitimishwa kwa wito wa mshikamano miongoni mwa wanachama wa TALGWU na
Serikali ili kuhakikisha changamoto zilizotajwa zinafanyiwa kazi kwa manufaa ya
wafanyakazi na maendeleo yao.
0 Comments