CCM YAPIGA HATUA KUELEKEA MIAKA 48

 



📌BAHATI MSANJILA

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kinakaribia kutimiza miaka 48 ya historia yake, na kwa heshima ya kumbukumbu hii muhimu, Jumuiya ya Wazazi CCM imepewa dhamana ya kuanzisha shamrashamra za maadhimisho hayo kwa kongamano maalum litakalofanyika tarehe 2 Februari 2024 jijini Dodoma.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhili Maganya, amesema kongamano hilo litawakutanisha wanachama, wananchi, na wakereketwa wa chama kwa lengo la kuangazia safari ya CCM—ilipotoka, ilipo sasa, na inapoelekea.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, tarehe 5 Februari 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, akiongoza hafla ya kihistoria itakayoakisi mafanikio ya chama na mchango wake kwa taifa.

Kwa mujibu wa Maganya, Profesa Palamagamba Kabudi, mmoja wa wanazuoni wakongwe na mashuhuri nchini, atakuwa miongoni mwa wachangia mada, akitoa uchambuzi wa kina kuhusu historia ya CCM na mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Maganya ametoa rai kwa wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kufuatilia vyombo vya habari kwa taarifa za kina kuhusu maadhimisho hayo.

 Pia, amewahimiza wanachama wa CCM na wananchi kushiriki kikamilifu katika kongamano hili ambalo linatarajiwa kuwa jukwaa la mijadala muhimu kuhusu mustakabali wa chama na taifa kwa ujumla.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Ally Hapi, amesema kongamano hilo litakuwa fursa muhimu ya kujadili historia ya CCM, mchango wake kwa taifa, na mustakabali wake katika kuimarisha maendeleo ya Tanzania.

Amesema kongamano litaangazia mchango wa CCM katika kujenga misingi ya demokrasia, mchango wa vijana na elimu kwenye maendeleo ya taifa pamoja na maadili na malezi.

Ameeleza kuwa mada zitakazojadiliwa zitagusa nyanja zote muhimu za maendeleo ya chama na taifa, huku akiwataka wananchi kufuatilia kwa karibu mjadala huo kupitia vyombo vya habari.





Post a Comment

0 Comments