BUNGE LAPITISHA AZIMIO LA KUMPONGEZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KWA MAFANIKIO YA MKUTANO WA NISHATI AFRIKA 2025

 



📌BAHATI MSANJILA

Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hii leo jijini Dodoma limeazimia Kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa Ufanisi wa Mkutano wa Nishati Afrika (Mission 300) wa Mwaka 2025

Katika kikao cha Bunge kilichofanyika tarehe 31 Januari 2025, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Azimio la kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa ya Mkutano wa Nishati Afrika (Mission 300) uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 27 - 28 Januari 2025.

Mkutano huo mkubwa wa kimataifa ulilenga kuweka mikakati ya kufikia umeme kwa watu milioni 300 Barani Afrika ifikapo mwaka 2030. 

 Akiliwasilisha azimio hilo, Mhe. Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, amesisitiza juhudi za kipekee za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mafanikio haya kwa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.

Mkutano huo umeleta manufaa kwa uchumi wa Tanzania, kwa kuhamasisha uwekezaji katika sekta mbalimbali, kama vile hoteli, usafiri, utalii, na biashara.

Aidha, mkutano huo umefanikisha kuanzishwa kwa Azimio la Dar es Salaam, ambalo linasisitiza umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030 na kuhamasisha nishati safi kwa wananchi, hasa wanawake.

Bunge limetambua juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na kumpongeza kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu kwa weledi na viwango vya kimataifa.

Pia, limepongeza mikakati madhubuti ya Rais ya kuhakikisha kuwa ifikapo 2030, Watanzania wote watakuwa na miundombinu ya umeme, na asilimia 75 ya Watanzania watakuwa wamepata nishati safi ya kupikia.

Bunge limeahidi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika dhamira yake ya kuwapatia Watanzania wote nishati ya umeme na nishati safi ya kupikia.

Azimio hili linaonyesha dhamira ya Bunge kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya nishati na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa Watanzania na kwa Bara la Afrika.

Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza taifa kwa ufanisi mkubwa, na mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa serikali, viongozi wa biashara, na mashirika ya kimataifa kutoka maeneo mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, na wadau wa nishati.





 


Post a Comment

0 Comments