TANZANIA YAJIDHATITI KWA MASHINDANO YA WABUNGE WA AFRIKA MASHARIKI MOMBASA

 ðŸ“ŒBAHATI MSANJILA

MWENYEKITI wa Klabu ya Michezo ya Bunge, Abas Tarimba, ameeleza maandalizi ya timu za Bunge la Tanzania kushiriki Mashindano ya Wabunge wa Afrika Mashariki, yatakayofanyika Mombasa, Kenya, mwezi Desemba 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Spika jijini Dodoma, Tarimba amesema mashindano hayo yanalenga kuimarisha mshikamano, ushirikiano, na afya za wabunge kupitia michezo mbalimbali.

Mashindano haya yanayoleta pamoja wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni fursa kubwa ya kuimarisha urafiki na mshikamano wa kikanda kupitia michezo. Timu zetu zinaendelea na maandalizi makali kuhakikisha tunaiwakilisha vyema nchi yetu

Tarimba.

Timu za Bunge la Tanzania zimekuwa zikiendelea na mazoezi jijini Dodoma kama sehemu ya maandalizi kabla ya safari ya kuelekea Mombasa tarehe 7 Desemba 2024. Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na soka, riadha, netiboli, na golf.

Mashindano haya, ambayo hufanyika kila mwaka, yanawakutanisha wabunge kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, na Tanzania.

Tarimba amesisitiza kuwa mashindano haya si tu kuhusu ushindani, bali pia ni nafasi ya kujenga afya na kuimarisha mahusiano ya kikanda kupitia michezo.

Tunawahimiza wabunge wote kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye maandalizi haya ili kuhakikisha tunarudi nyumbani na ushindi, lakini zaidi ya yote, tuendeleze mshikamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mashindano haya yanatarajiwa kuwa kivutio kikubwa na yataonyesha umuhimu wa michezo katika kujenga uhusiano wa kisiasa na kijamii miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki.



 

Post a Comment

0 Comments