VIJANA WA BODABODA DODOMA WANUFAIKA NA MCHANGO WA UVCCM

 





📌 BAHATI MSANJILA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Cde. Jokate Mwegelo, ameonyesha tena nia ya kuimarisha ustawi wa vijana nchini kwa kuchangia Shilingi milioni tatu kwa bodaboda wa kituo cha Sabasaba A, maarufu kama “Vijana na Samia,” mkoani Dodoma.

 

Mchango huo unalenga kuwawezesha vijana hao kuboresha huduma zao na kuimarisha mfuko wa maendeleo wa kituo hicho. Uzinduzi wa shina la Wakereketwa la UVCCM la “Vijana na Samia” ulifanyika sambamba na kukabidhiwa kibanda maalum kwa ajili ya kupumzikia, kilichojengwa kwa msaada wa Mbunge wa Dodoma Mjini, Ndg. Anthony Mavunde.

 

Akizungumza katika tukio hilo, Cde. Jokate aliwataka vijana hao kuendelea kuwa na imani na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha juhudi kubwa zinazofanyika kuhakikisha vijana wanapewa nafasi na msaada wa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.

 

Serikali ya Rais Samia imejikita katika kuwawezesha vijana, na nyinyi ni sehemu muhimu ya mabadiliko hayo. Endeleeni kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi hizi,


Kabla ya tukio hilo, Cde. Jokate aliongozana na vijana zaidi ya 500 waliokuwa wakihamasisha maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum wa CCM unaotarajiwa kufanyika Januari 18 hadi 19, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete. Vijana hao walionyesha mshikamano na hamasa kubwa, wakiendelea kuipa nguvu kauli mbiu ya chama “Kijana na Kijani.”

 

Mbunge wa Dodoma Mjini, Ndg. Anthony Mavunde, alisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi kwa vijana na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kwa karibu. Kibanda cha kupumzikia kilichozinduliwa sasa kitasaidia bodaboda kujikinga dhidi ya jua na mvua wakati wa shughuli zao za kila siku.

 

Uzinduzi wa shina hilo ni moja ya hatua muhimu za UVCCM katika kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na kuimarisha mshikamano ndani ya chama.






 


Post a Comment

0 Comments