VETA KUANDAA KIKAO CHA WADAU WA HUDUMA YA UKARIMU NA UTALII DODOMA

 ðŸ“ŒBAHATI MSANJILA

MKURUGENZI wa VETA Kanda ya Kati, Ramadhan Matata, ametangaza kuwa tarehe 29 Novemba 2024 kutakuwa na kikao muhimu cha wadau wa sekta ya huduma ya utalii na ukarimu  mkoani Dodoma.

Lengo la kikao hicho ni kujadili namna ujuzi unaotolewa na watoa huduma unavyoweza kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya wamiliki wa hoteli na wageni wanaopata huduma hizo.

Amesema kuwa Mkutano huo, utakaofanyika kwa ushirikiano kati ya VETA na wadau wa sekta hiyo, utahusisha majadiliano kuhusu changamoto zinazowakabili watoa huduma, fursa zilizopo, na mikakati ya kuboresha huduma.

Miongoni mwa changamoto kubwa zilizotajwa ni utovu wa nidhamu, ukosefu wa uaminifu, na maadili yasiyoridhisha kutoka kwa baadhi ya wahudumu wa hoteli, ambao hawajapata mafunzo rasmi.

Matata ameongeza kuwa kupitia kikao hicho pia VETA inalenga kuziba pengo hili kwa kuanzisha kozi fupi za mafunzo kwa vijana wasioajiriwa rasmi, ili kuwawezesha kufanikisha viwango vya juu vya huduma.

Mkurugenzi Matata amesema kozi hizo fupi za mafunzo kwa vijana ambao hawana ajira rasmi zitawawezesha kupata ujuzi unaohitajika katika sekta ya ukarimu, Mpango huo unalenga kuimarisha huduma zinazotolewa na wahudumu wa hoteli, kuhakikisha wanakidhi matarajio ya wateja.

Kikao hiki kinatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya ukarimu na utalii mkoani Dodoma. Kupitia ushirikiano wa wadau na VETA, huduma bora, zenye viwango, na zinazoendana na soko zinatarajiwa kuwa sehemu ya kawaida ya sekta hii.

Wadau wote wanakaribishwa kushiriki kikao hiki na kuwa sehemu ya mabadiliko yenye manufaa kwa sekta ya ukarimu na utalii nchini Tanzania

Post a Comment

0 Comments