📌BAHATI MSANJILA
Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kimeendelea kuthibitisha nguvu yake kwenye siasa za ndani kwa kushinda zaidi ya
asilimia 98 ya nafasi zote tano zilizogombewa katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024. Matokeo haya yameacha vyama vingine 11
vikijikongoja na kushinda chini ya asilimia 2, huku vyama saba kati ya vyama 19
vilivyoshiriki vikishindwa kabisa kupata nafasi yoyote.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ametangaza matokeo hayo jijini Dodoma,
akieleza kuwa nafasi zilizogombewa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji,
Mwenyekiti wa Kitongoji, Mwenyekiti wa Mtaa, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji,
na Wajumbe wa Kamati za Mtaa. Kulingana na taarifa hiyo, wapiga kura milioni
26.9, sawa na asilimia 86.3 ya waliojiandikisha, walijitokeza kushiriki
uchaguzi huu muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya jamii za mitaa.
Mtakumbuka kuwa uchaguzi huu ulitanguliwa na mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kati ya Oktoba 26 hadi Novemba 1, 2024, ambapo wagombea walichujwa kupitia vigezo mbalimbali hadi kufikia jumla ya wagombea walioteuliwa kwa kila nafasi
Waziri Mchengerwa.
Katika nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji, CCM imejinyakulia ushindi wa asilimia 99.01, huku nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa ikishuhudia chama hicho kikishinda asilimia 98.83. Vyama vya upinzani kama CHADEMA, ACT-Wazalendo, na CUF vimeambulia idadi ndogo ya ushindi, vikibaki na nafasi chache katika miji na vijiji.
Uchaguzi huu, ulioendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Serikali za Mitaa, pia umeonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi, ambapo asilimia 86.36 ya waliojiandikisha walipiga kura licha ya changamoto kama pingamizi na kasoro nyingine ndogo ndogo katika baadhi ya maeneo.
0 Comments