📌RHODA SIMBA
Serikali imesema kwa kutambua umuhimu wa Maji kwa ajili ya wananchi wake, inaendelea kutekeleza miradi mikubwa miwili ya kutoa maji Ziwa Victoria ambayo ni Mradi wa Ziba-Nkinga wenye kuhudumia vijiji 9 na Mradi wa Nkinga Simbo utakaohudumia vijiji 8 vilivyopo jimbo la Manonga Mkoani Tabora.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Manonga Seif Gulamali, aliyeuliza lini Serikali itatenga Fedha za ujenzi wa Miradi ya maji ya Ziwa Victoria katika kata ya Igoweko, Uswayu na Tambalale - Manonga.
Mhandisi Kundo amesema Mipango ya Serikali ni kusambaza maji kupeleka katika Kata za Igoweko, Tambalale na Uswayu mara baada ya kukamilisha miradi hiyo.
Amesema Serikali inaendelea na zoezi la uchimbaji visima na kujenga miundombinu rahisi ya kuchotea maji (Point source) kwa vijiji vya Igoweko, Mpogolo na Igondela vilivyoko katika kata ya Igoweko.
0 Comments