📌 RHODA SIMBA
Serikali itaendelea kuboresha bajeti ya Mamlaka ya usimamizi wa
wanyamapori(TAWA), Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro(NCAA) na Shirika la Hifadhi za
Taifa(TANAPA) kutegemeana na hali ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili
kuimarisha shughuli za ulinzi na kuboresha miundombinu ya utalii.
Haya yamebaishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akijibu swali la Mhe. Esther Edwin Malleko(Mb) aliyetaka kujua kuna mkakati gani wa kuwaongezea bajeti TANAPA na TAWA kwani majukumu yao ni makubwa ikilinganishwa na bajeti inayotengwa.
Mhe. Kitandula alisema kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali iliziongezea taasisi za uhifadhi bajeti ya matumizi ya kawaida (OC). Mathalan, bajeti ya TANAPA iliongezwa kutoka Shilingi 106,958,705,429.41 ya mwaka 2022/2023 hadi kufikia Shilingi 118,307,272,800.00 ikiwa ni ongezeko la shilingi 11,348,567,370.59 sawa na ongezeko la asilimia 10.61.
Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa baada ya janga la ugonjwa wa UVIKO - 19 mwaka 2019, ambalo liliathiri shughuli za utalii kwa kiasi kikubwa, taasisi za uhifadhi hususan TANAPA pamoja na TAWA zilishindwa kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kujiendesha hali ambayo iliifanya Serikali kuchukua hatua za makusudi za kunusuru taasisi hizo kwa kugharamia uendeshaji pamoja na kulipa mishahara ya watumishi.
Kufuatia hatua hizo, hadi sasa taasisi za uhifadhi (TANAPA, TAWA na NCAA) zinapata fedha za uendeshaji kutoka Serikalini kulingana na ukomo wa bajeti uliopangwa na kuidhinishwa.
0 Comments