NMB YATOA VIFAA VYA MILLIONI 56.7 MTWARA NA MOROGORO

 




📌BAHATI MSANJILA

Katika kuhakikisha benki ya NMB inaendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wake katika sekta ya Elimu na Afya  imetoa vifaa mbalimbali katika shule za msingi, Sekondari pamoja na Zahanati katika Mikoa ya Morogoro na Mtwara.

Vifaa hivyo ambavyo vimegharimu kiasi cha Sh Milioni 56.7 ni pamoja na madawati 219 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi za Mafisa ‘A’ iliyoko Manispaa ya Mororgoro, Shule za Msingi za Njengwa na Mbemba za Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoani Mtwara.

Vifaa vingine ni Meza pamoja na Viti 220 vilivyotolewa kwa ajili ya Shule za Sekondari za Kingo Manispaa ya Morogoro na Shule za Sekondari za Mtiniko, Mnongodi na Nyundo zote za Halmashauri ya Mji Nanyamba Mtwara.

Katika sekta ya Afya NMB imetoa vitanda 10 na magodoro 10 kwa ajili ya wagonjwa na vitanda viwili maalumu kujifungulia wajawazito, vifaa ambavyo vilitolewa ili kutoa huduma katika Hospitali ya Wilaya Nanyamba Mtarwa.

Aidha Benki hiyo ilikabidhi magodoro 26 kwa ajili ya kuboresha huduma katika vituo vya Afya vya Dinyecha pamoja na Nyundo katika Halmashauri hiyo ya Mji wa Nanyamba Mkoani Mtwara.

Akiwa Mkoani Morogoro kukabidhi vifaa hivyo Afisa Mkuu Wateja Wakubwa na Serikali Benki ya NMB, Alfred Shao alisema kuwa sekta za Afya na Elimu ni maeneo ya kipaumbele kwa NMB, ambapo utumia asilimia moja ya faida ili kusaidia utatuzi wa changamoto kwenye jamii

 Tulipopata maombi haya ya kuchangia maendeleo ya vituo vya kutolea huduma za Afya na shule katika Wilaya hii, tulifarijika na kuamua mara moja kuja kushirikiana na serikali ili kuwa chachu ya maendeleo ya sekta hizo muhimu kwa jamii yetu,

Aidha Meneja huyo alieleza kuwa serikali imekuwa ikifanya mambo makubwa katika kuwaletea watanzania maendeleo, ambapo NMB kama mdau mkubwa umekuwa wajibu wao katika kuunga mkono juhudi hizo za kuhakikisha huduma za kijamii zinaboreshwa zaidi.

Mkoani Mtwara Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Olipa Hebel alisema kuwa Changamoto za Afya na Elimu kwa NMB ni jambo la kipaumbele kutokana na Nyanja hizo kuwa ndizo msingi wa maendeleo kwa taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, Katibu wa kituo cha afya cha Dinyecha, Hamisi Hassan aliishukuru benki ya NMB kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo alisema vitawasaidia kwani ni vifaa muhimu.

 Ukiviangalia ni vya kisasa na sasa mama wajawazito watajifungua kwa usalama zadi na itatupunguzia kero ya upungufu wa vifaa tiba katika Halmashauri yetu na tunawakaribisha wadau wengine waje watoe misaada

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Nanyamba ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kitaya, Kapende Jamali Abdallah, alishukuru NMB kwa kuwaunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma kwenye sekta hizo.

 Hadi kufikia leo ni miaka saba mfululizo benki hii imekua ikituunga mkono katika sekta za elimu, afya na maafa na ninaomba wasituchoke

 


Post a Comment

0 Comments