BARABARA YA KARAMBA-NDEA KUBORESHWA ILI IWEZE KUTUMIKA MWAKA MZIMA

 



📌RHODA SIMBA

Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga fedha kiasi cha Shilingi milioni 78 kwa ajili ya kuiboresha barabara Karamba-Ndea yenye urefu wa kilometa 18 kwa kiwango cha changarawe ili kuwezesha barabara hiyo kutumika kwa shughuli za utalii katika msimu mzima wa mwaka. 

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Mhe. Joseph Anania Tadayo aliyetaka kujua Serikali itafungua lini na kuanza kutumia lango la Kaskazini la Hifadhi ya Taifa Mkomazi lililojengwa Ndea wilayani ya Mwanga.

Aidha Wizara ya Maliasili na Utalii ipo katika hatua mbalimbali za kufanya maboresho ya miundombinu ya utalii pamoja na kuongeza malango ya wageni ili kufanikisha watalii kufika katika vivutio vilivyopo kwenye Hifadhi za Taifa Tanzania ikiwemo Hifadhi ya Taifa Mkomazi.

Kwa sasa ujenzi wa lango la kupokelea wageni katika eneo la Ndea ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi umekamilika. Pia, barabara inayounganisha Hifadhi ya Taifa Mkomazi kupitia lango hilo na Wilaya ya Mwanga imeshafunguliwa.

 


Post a Comment

0 Comments