📌BAHATI MSANJILA
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, Oktoba 24, 2024, amezindua miradi miwili yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 436.4 katika wilaya ya Mkalama, mkoani Singida. Miradi hiyo inajumuisha mradi wa maji na zahanati, ambayo itasaidia kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hilo.
Mradi wa maji uliozinduliwa katika kijiji cha Nkalakala umegharimu shilingi milioni 348.9 na Utekelezaji wa mradi huu utasaidia kupunguza changamoto kubwa ya wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Christopher Saguda, alisema tanki hilo lina uwezo wa kuhifadhi lita 90,000 na litahudumia vituo 12 vya kuchotea maji na Ujenzi wa tanki hilo umekamilika kwa asilimia 100.
Aidha, Waziri Silaa alizindua zahanati ya Igonia iliyopo kijiji cha Mtogo Mwili, iliyogharimu shilingi milioni 87.4. Zahanati hii ilianza kujengwa kwa michango ya wananchi kabla ya serikali kuendeleza ujenzi wake. Huduma zitakazotolewa katika zahanati hiyo zitahudumia vijiji vya Igonia, Ikungu, na Mtamba, ikinufaisha wananchi 1,408 kulingana na sensa ya mwaka 2022.
Huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za wagonjwa wa nje na uzazi.
Katika hatua nyingine, Waziri Silaa alikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) katika kijiji cha Mwando, ambao umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.4. Chuo hiki kitatoa mafunzo ya ufundi kwa vijana, na hivyo kusaidia kukuza ujuzi na ajira katika jamii.
Wananchi wa wilaya ya Mkalama wameeleza shukrani zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi hii ya maendeleo, ambayo itaboresha miundombinu na huduma za kijamii katika eneo hilo.
0 Comments