WAKUU WA MAMLAKA YA KUPAMBANA NA RUSHWA UKANDA WA SADC WAKUTANA NCHINI ZAMBIA

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU , Crispin Francis Chalamila ambaye pia ni Mwenyekiti mpya wa Kamati ya SADC ya kupambana na Rushwa (SACC)
 

📌MWANDISHI WETU

WAKATI Dunia ikishuhudia majanga katika maeneo mbalimbali, Mamlaka za Kupambana na Rushwa ukanda wa SADC zimetahadharishwa kuwa makini kwani mikakati ya haraka inayoandaliwa kukabiliana na hali hiyo inaweza kutoa mianya ya rushwa.

Akizungumza Oktoba 2, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa mamlaka hizo Jijini Lusaka - Zambia, Mwenyekiti mpya wa Kamati ya SADC ya Kupambana na Rushwa (SADC Anti Corruption Committee - SACC) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini - TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, amefafanua kuwa hatari ya uwepo wa vitendo vya rushwa inaweza kujitokeza wakati wa mchakato wa kupata na au kutoa misaada wakati wa dharura.

Hatua zote za mnyororo wa utoaji wa misaada ziko katika hatari ya rushwa kutokana na dharura inayokuwepo

Katika Mkutano huo unaoongozwa na kaulimbiu “Kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika usimamizi wa majanga na huduma za magereza katika ukanda wa SADC”, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alitaja aina za vitendo vya rushwa vinavyoweza kutokea katika mazingira hayo ya ‘udharura’ kuwa ni pamoja na udanganyifu, ubadhilifu wa misaada, kuingilia usajili wa walengwa, utendaji usio wa maadili katika ununuzi na kwamba pia hali hiyo inaweza kusababisha matumizi mabaya ya ngono

Mkurugenzi Mkuu amesema mlipuko wa magonjwa na mabadiliko ya tabia nchi unaongeza hali za dharura huku akisisitiza

Hali hii inasababisha umuhimu wa kuwa na mikakati ya kudhibiti vitendo vya Rushwa katika ushughulikiaji na usimamizi wa dharura za majanga

Mkurugenzi Mkuu pia amewashukuru nchi wanachama kwa ushirikiano na uungaji mkono wa juhudi za kikanda za Kuzuia na Kupambana na Rushwa na amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zambia, Monica Chipanta Mwansa (ambaye ni mwenyekiti aliyemaliza muda wake), kwa maendeleo yaliyopatikana wakati wa kipindi chake cha uongozi na hususani katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa SADC wa Kupambana na Rushwa (2023-2027), ambao unatekeleza malengo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa nchi za SADC.

Mkutano huu wa siku tatu umehudhuriwa na nchi wanachama wa SADC 14, huku Tanzania ikiongoza mapambano hayo kwa mara ya pili baada ya kuwa Mwenyekiti mwaka 2017/2018.

Wakuu wa Mamlaka za Kupambana na Rushwa ukanda wa SADC pamoja an wajumbe ana viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja


 

Post a Comment

0 Comments