ZAIDI YA WAKULIMA 700 KUNUFAIKA NA MATREKTA YA NEW HOLLAND NA PASS LEASING

 

📌RHODA SIMBA

WAKULIMA takribani 700, wanatarajia kunufaika na matrekta ya New Holland kwa kushirikiana na PASS Leasing ambao wamegawa vifaa mbalimbali vya kilimo ikiwemo matrekta ,Lori la kubebea Mizigo pamoja na mashine ya kuchakata mazao mbalimbali kwa wakulima 12 kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dodoma. 

Akikabidhi matrekta hayo katika viwanja vya maonesho vya Nanenane jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema hatua hiyo ni mapinduzi makubwa ambayo yanaendana na dhamira ya Rais ya kuwawezesha wakulima kupata vifaa vitakavyowasaidia katika shughuli zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Leasing, Killo Lussewa, ameeleza kuwa ni moja ya majukumu yao kuwasaidia wakulima ambapo hadi sasa takriban wakulima 1200 wamefikiwa.

Boniface Mollel, Afisa Masoko wa Highes Agriculture Limited, amesema kuwa wakulima waliopewa matrekta hayo pia watapewa na vifaa vya ziada ambavyo vitawasaidia kwajili ya matengenezo.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa matrekta hayo, Minza Mlela, mkulima kutoka Chamwino, amesema matrekta hayo yatawasaidia kufanya kazi za kilimo kwa haraka na yatawaongezea kipato kwa kuyakodisha kwa wakulima wengine.

 

 


Post a Comment

0 Comments