KATAMBI - TANZANIA KUADHIMISHA SIKU YA VIJANA



📌RHODA SIMBA

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Patrobass Katambi amesema kuwa jumla ya Vijana elfu 3,000 kutoka katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar, wataadhimisha Siku ya Vijana ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya vijana

Katambi ameyasema hayo Agosti 9 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Vijana ya Kimataifa ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa na jamii kwa ujumla kupata fursa ya pamoja ya kusherehekea na kutambua nafasi na mchango wa vijana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye nchi zao, na Tanzania ikiwemo.

Waziri huyo amesema kupitia kongamano hilo, vijana watajadili masuala mbalimbali ikiwemo; kutoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo (Tanzania tuitakayo 2050), vijana na matumizi ya fursa za kidijitali, vijana na uchumi, afya ya akili, na saikolojia ya vijana. 

Kabla ya maadhimisho hayo shughuli zitakazotekelewa ni pamoja na Agosti 10 na 11, 2024 kutakuwa na kongamano la vijana litakalofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

 

Na kuogeza Agosti 12, 2024, itakuwa ni siku ya kilele cha kuadhimisha Siku ya Vijana Kimataifa, ambapo vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana watashiriki. Mgeni rasmi wa maadimisho ya mwaka huu anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb)  Ameeleza

 

Amebanisha kuwa, Kilele cha maadhimisho hayo kitaambatana na uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, toleo la mwaka 2024. Sera hii pamoja na mkakati wa utekelezaji wake ni nyenzo muhimu kwa wadau wa maendeleo ya vijana nchini.

 

Itambulike kwamba, vijana ndio kundi kubwa, na kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15-35 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 21,312,411 sawa na (34.5%) ambapo kwa Tanzania bara ni 20,612,566 sawa na (34.4%).

 

Kwa kutambua kuwa vijana ndio nguvu ya kufanya kazi, wabunifu na chachu ya mabadiliko katika jamii yoyote ile. Pia Vijana ndiyo warithi wa historia katika Mataifa yao. Kwa mantiki hii hatuna budi kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika maendeleo ya nchi yetu,  Amesema Katambi.

 

 


Post a Comment

0 Comments