SERIKALI imesema ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma kimekamilika kwa asilimia 99, huku safari zikitarajia kuanza Alhamisi Julai 25 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema hivi sasa wanaendelea kukamilisha vitu vichache ili ifikapo Julai 25 mwaka huu safari zianze rasmi.
Hivi sasa tumefikia asilimia 99 na wataalamu wetu wanamalizia vitu vichache ili safari zianze rasmi siku ya Alhamisi Julai 25 mwaka huu. Tumeweka utaratibu mzuri kwa wananchi kukata tiketi kwa njia ya mtandao ili kurahisisha mambo
Ameongeza kuwa:"Baada ya kukamilisha kazi zote Wizara inaendelea kuweka utaratibu ili Rais Dk Samia aweke jiwe la msingi la kuzindua rasmi safari za treni ya mwendo kasi
Kadogosa amewahamasisha viongozi wa Kimila kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutunza miundombinu ya SGR kwani serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia ujenzi wake.
Viongozi wa Kimila wakiwemo Machifu ni viongozi muhimu hasa katika ulinzi wa miundombinu ya reli. Niendeelee kuwaomba ndugu zetu muendelee kutoa elimu kwa wananchi faida ya reli hii hasa katika kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla
Kwa upande wake Chifu kutoka Dodoma Chifu Mazengo alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo SGR ambapo kukamilika kwake kutaifungua nchi Kitaifa na Kimataifa.
Amewasisitiza wananchi wanaozunguka miradi mikubwa ya kimkakati kuendelea kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao kujikwamua kiuchumi.
0 Comments