SAMIA SCHOLARSHIP EXTENDED YATENGA BILIONI 1.6 UFADHILI MASOMO YA CHUO KIKUU



📌RHODA SIMBA

WAZIRI wa Elimu Sayansi,na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema,kupitia Tume ya nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imetangaza kutoa ufadhili wa masomo ya Chuo Kikuu nje ya nchi kwa asilimia miamoja kwa shahada za umahiri (MSc) katika fani za sayansi na teknolojia ya nyuklia. 

Prof. Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema Mwaka huu wa Fedha 2024/2025 Samia Scholarship Extended imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 1.6 kuwezesha mpango huo.

Aidha ameeleza kwamba Serikali inafanya uwekezaji kwenye Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kukidhi mahitaji makubwa ya huduma zitokanazo na Teknolojia ya nyuklia na upungufu wa wataalamu hapa nchini. 

Wizara imebaini ongezeko kubwa la matumizi haya hasa kwenye miradi mikubwa ya madini kama vile Urani, Madini Adimu na maeneo mengine ambayo yanahitaji nchi kuwa na wataalamu wa ndani na wabobezi kwelikweli

Mkenda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mionzi Tanzania (TAEC) Prof. Najat Mohamed, amesema ufadhili unalenga eneo la Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia katika; matibabu ya saratani, utafiti wa maji, hewa na mimea, unururishaji wa vifaa tiba, bidhaa za viwandani na mazao, nishati ya nyuklia na utafiti wa vinu vya nyuklia pamoja na uzalishaji wa dawa za mimea.

Amesema ufadhili huo utatolewa kwa waombaji wenye sifa katika Vyuo Vikuu vinavyotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwenye nchi za Australia, Austria, Ubelgiji, Canada, China, Jamhuri ya Czech, Sweden, Ufaransa, India, Korea ya Kusini, Uturuki, Urusi, Finland, Uingereza na Marekani.



Post a Comment

0 Comments