WIZARA YA ULINZI YAELEZEA MAFANIKIO MIAKA 60 YA MUUNGANO.

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Stergomena Tax amesema kuwa Kimataifa na Kikanda, Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuhakikisha hali ya Ulinzi na Usalama inaimarika.

Hayo ameyasema leo April 3 2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Muungano. 

Amesema kuwa kwa sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia JWTZ inashiriki katika operesheni mbalimbali za Umoja wa mataifa kwa kutoa vikosi vya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati, Sudan Kusini, na Lebanon.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia JWTZ pia inashiriki katika operesheni za kuleta amani nchini Msumbiji kupitia Misheni ya SADC (SADC Mission in Mozambique - SAMIM) iliyopo chini ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Misheni ya kuleta Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC) iliyopo chini ya SADC

Tax

JWTZ imeendelea kutoa maafisa wanadhimu wakuu katika misheni za Umoja wa Mataifa na misheni za Kikanda.

Tunapoadhimisha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Ulinzi na JKT inayo kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu zote sita (6) za uongozi, Awamu ya kwanza ilijenga nchi, umoja wa kitaifa, iliunda Jeshi, iliandaa vijana kwa ulinzi wa nchi yao ambao walimshinda “Nduli Iddi Amin Dadaa"

Kadhalika amesema kuwa Katika kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru, na usalama wa nchi, Wizara kupitia JWTZ imechangia katika kujenga uchumi imara ambapo wananchi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu. 

Amesema yote hayo yamewezekana kutokana na kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mipango madhubuti katika ulinzi wa nchi, vinavyotoa fursa kwa wananchi kujikita katika ujenzi wa Taifa lao. 

Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara imeendelea kutekeleza, na kuliimarisha Jeshi kwa kulipatia zana na vifaa bora na vya kisasa, rasilimali watu na nyenzo za kufanyia mazoezi ili kuwa imara wakati wote kwani Mwaka 1966 Serikali iliandaa sheria ya ulinzi wa Taifa (National Defence Act (NDA)).

Ili kuliimarisha Jeshi, Serikali kupitia Wizara imeendelea kuboresha maslahi kwa Wanajeshi na Watumishi wa Umma kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu, kwa kuwapatia makazi bora kwa kuwajengea nyumba, pamoja na stahili mbalimbali, kupandisha vyeo kulingana na sifa, vigezo na taratibu. 

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni Miongoni mwa Wizara zinazotekeleza masuala ya muungano.





 

Post a Comment

0 Comments