MAJALIWA AELEZA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA UHABA WA SUKARI NCHINI

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA 

SERIKALI imesema ili kukabiliana na uhaba wa sukari uliojitokeza nchini, imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa vibali vya kuagiza tani 100,000 za sukari kutoka nje ya nchi ambapo hadi tarehe 15 Machi, 2024, jumla ya tani 32,085.50 kati ya tani 100,000 zilizoidhinishwa zimeingizwa nchini na usambazaji unaendelea. 

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo April 3, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba kuhusu, mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya bunge.

Amesema mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka 2023/2024 ni wastani wa tani 807,000 ambapo matumizi ya kawaida ni tani 552,000 na mahitaji kwa ajili ya matumizi ya viwandani ni tani 255,000. 

Katika kipindi hicho uzalishaji wa sukari kwa ajili ya matumizi ya kawaida ulikadiriwa kufikia tani 555,000, wakati uzalishaji halisi ulikuwa tani 367,487.54 sawa na asilimia 66.2 ya lengo.

Kutofikiwa kwa lengo la uzalishaji kulitokana na mvua za El-Nino kuanzia mwishoni mwa mwaka 2023 ambazo zilileta athari katika uzalishaji kutokana na maji kujaa kwenye mashamba ya miwa na hivyo kuathiri shughuli za uvunaji miwa na kusimama kwa uzalishaji wa sukari katika viwanda vya TPC, Mtibwa, Bagamoyo na Kiwanda cha K1 cha Kampuni ya Sukari Kilombero tangu mwanzoni mwa Novemba 2023.

Hali hiyo ilisababisha upungufu wa sukari na hivyo bei ya bidhaa hiyo kupanda katika maeneo mengi nchini

Majaliwa

Post a Comment

0 Comments