KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi
Mwajuma Waziri amezindua ripoti ya 15 ya utendaji wa Mamlaka za Majisafi
na Usafi wa Mazingira nchini iliyoandaliwa na Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA).
Akizungumza leo Machi 18, 2024 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo Mhandisi Mwajuma amewaagiza wakurugenzi wa Mamlaka za majisafi nchini kuhakikisha kuwa wanatatua tatizo la upotevu wa maji nchini kwani kiasi kinachotakiwa ni asilimia 20 lakini kuna baadhi ya mamlaka zinapoteza asilimia 37.2 za maji yanayozalishwa.
Amesema kiasi hicho ni kikubwa na kinaathiri upatikanaji wa huduma za majisafi kwa wananchi hivyo hatua za mapema zichukuliwe ili kupunguza kiwango hicho cha upotevu wa maji.
Nazitaka mamlaka hizo kutoa elimu kwa jinsi ya kuvuna maji ya mvua kwaajili ya matumizi wakati wa ukame kwani maji mengi ya mvua huwa yanapotea na kusababisha madhara kwenye miundombinu ambayo yakivunwa yatasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa maji nchini.
Mhandisi Waziri
Aidha amesema kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030 na hususan Lengo Namba 6 linaeleza umuhimu wa Majisafi na Usafi wa Mazingira.
Amesema kuwa lengo hilo linasisitiza kuhakikisha uwepo na usimamizi endelevu wa maji na usafi wa mazingira kwa wote ikiwa ni pamoja na watu wote kuwa na uhakika wa upatikanaji wa majisafi na salama ya kunywa kwa bei nafuu ifikapo mwaka 2030.
EWURA inategemewa katika utekelezaji wa lengo hili ukiacha wadau wengine kwani ndiyo iliyopewa dhamana ya udhibiti wa sekta hii nyeti. Tumeshuhudia tangu EWURA ianze kuzisimamia mamlaka za maji nchini, kumekuwa na maboresho ya utendaji wa mamlaka hizi. Ni kwa msingi huu, naendelea kuipongeza EWURA na kuitaka iendelee kufanya kazi ya udhibiti kwa uwazi, ufanisi, weledi na tija kama ilivyoainishwa kwenye dhamira ya kuanzishwa kwake ili pia kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza Ilani
Mhandisi Waziri
Amesema kuwa Taarifa hiyo inaonesha kuimarika kwa baadhi ya viashiria vya utendaji kwenye Mamlaka za Maji ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha 2021/22 na kuzipongeza mamlaka za maji kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi wao katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Pia amezitaka Mamlaka za Maji kuzingatia miongozo mbalimbali ya kudhibiti upotevu wa maji ambayo hutolewa na EWURA kama vile Mwongozo wa kupunguza upotevu wa maji wa mwaka 2021 ambao unazitaka Mamlaka za Maji kuandaa mizania ya kupima viwango vya upotevu wa maji kwa mujibu wa mwongozo wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wataalam wa Maji (IWA).
Pamoja na kumairika kwa baadhi ya viashiria vya utendaji wa mamlaka za maji ambavyo baadhi nimevitaja hapo awali, nimesikitishwa na kuendelea kuzorota kwa baadhi ya viashiria hivyo pamoja na kushindwa kufikiwa kwa malengo ambayo mamlaka hizo zilijiwekea
Taarifa inaonesha kuwa, upotevu wa maji dhidi ya kiwango cha maji kinachozalishwa umeongezeka kutoka asilimia 35.5 mwaka 2021/22 hadi kufikia asilimia 37.2 mwaka 2022/23. Ndugu zangu hii haikubaliki hata kidogo. Sote tunajua kiwango cha upotevu wa maji kinachokubalika ni chini ya asilimia 20. Ni lazima mamlaka za maji ziweke na kutekeleza mikakati ya kuhakikisha zinapunguza kiwango cha upotevu wa maji
Mhandisi Mwajuma
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile amesema taarifa iliyozinduliwa leo ni ya 15 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo miaka 18 iliyopita na inahusisha uchambuzi wa utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 85 zikiwemo; mamlaka 25 za mikoa, saba (7) za miradi ya kitaifa, 47 za wilaya na Sita (6) za miji midogo.Dkt.Andilile amesema kuwa kwa ujumla, utendaji wa mamlaka za maji na usafi wa mazingira umeendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022/23, Mamlaka za Maji 78 kati ya 85 zilipata alama kuanzia wastani hadi vizuri sana katika utendaji wa ujumla ikilinganishwa na mamlaka 77 kati ya 90 kwa mwaka 2021/22.
Aidha amesema mafanikio mengine yaliyofikiwa ni
kuimarika kwa uwiano wa maunganisho yaliyofungwa dira za maji kufikia asilimia
92 ikilinganishwa na asilimia 90, Kuongezeka kwa kiwango cha ubora wa maji
yanayosambazwa kwa wateja kutoka asilimia 91 hadi 94 na kuongezeka kwa wateja
wa maji wa majisafi kutoka 1.3 hadi 1.5
Amesema pia kumekuwa na ongezeko la wateja wa mtandao wa uondoaji majitaka kutoka wateja 55,996 hadi wateja 56,899 sawa na asilimia 16 japo bado kuna uchache wa miundombinu ya kutibu majitaka na topetaka
Naomba nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wewe Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi wako mahiri wa sekta ya maji kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani na kuimarisha ustawi wa watanzania wote, kwani maji ni UHAI.
Dkt. Andilile
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) Omar Ali Yussuf,amesema kuwa EWURA imekuwa ikifanya kazi kubwa ambayo inaleta heshima kwa taifa la Tanzania.
Niseme tu wazi kwamba EWURA imekuwa ni kioo kwa nchi nyingi sana za Afrika mashariki, tumekuwa tukipata hizi katika maeneo ambayo tumekuwa tunakwenda lakini nyie wenyewe pia ni mashahidi kwa wale ambao wanakuja kujifunza kupitia kwenu nyie
Pia amesema kuwa suala la maji ni suala ambalo linamgusa kila kiumbe hai katika dunia pia alisema kuwa jamii yote inahitaji maji hivo suala la maji ni suala muhimu katika Nchi.
Uzinduzi huo umekwenda sambamba na utoaji wa tuzo mbalimbali kwa Mamlaka zilizofanya vizuri huku zikigawanywa katika makundi Matatu tofauti kulingana na idadi ya wateja inayowahudumia ambapo kundi la kwanza ni Mamlaka za maji zenye wateja chini ya 5000, kundi la pili ni mamlaka za maji zenye wateja chini kati ya 5000 na 20,000 na kundi la Tatu ni mamlaka za maji zenye wateja zaidi ya 20,000.
0 Comments