WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali kupitia wizara hiyo imepanga kuanza ujenzi wa barabara kwa ushirikiano wa Sekta Binafsi na Umma (PPP) ili kuharakisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameeleza hayo Bungeni jijini Dodoma leo Februari 5, 2024 wakati akiwasilisha majibu ya Wizara hiyo kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokuwa ikieleza Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023/2024.
Tutajenga miundombinu ya barabara kwa kushirikiana na wabia katika mfumo wa PPP, hii itaisaidia serikali kuhakikisha inakuwa na miundombinu bora, na kwa sasa tunaanza na Barabara ya Dar es Salaam - Dodoma ambayo itakuwa ni barabara ya ‘Express Way’, ujenzi wa barabara hii utasaidia pia kupunguza foleni
Bashungwa.
Kuhusu uwezeshaji wa Wakandarasi wazawa, Waziri Bashungwa amesema aliunda Kamati ya kuchambua mapungufu yaliyopo kwa Wakandarasi wazawa ikiwa ni pamoja na mitaji, mitambo, uwezo wa kusimamia miradi ambapo kamati hiyo imeshakamilisha taarifa ya awali ambayo itawasilishwa katika Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.
Kadhalika, Bashungwa amewaondoa wasiwasi Wabunge juu ya utekelezaji wa miradi ya EPC+F ambapo amesema Wakandarasi 7 wanaotekeleza miradi hiyo wanafanya mapitio upembuzi yakinifu uliofanywa na Wakala wa Barabara (TANROADS) mwaka 2017 ili kupata taarifa halisi za ujenzi wa barabara hizo na ukikamilika miradii itaanza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso (Mb) amesema Serikali ione umuhimu wa kuiongezea bajeti Wizara hiyo ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi nchini ikiwemo barabara na madaraja.
Amesema Kamati imependekeza kuwa Serikali iongeze kiasi cha shilingi Trilioni 5 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili iweze kusaidia utekelezaji wa ujenzi na matengenezo ya barabara nchi nzima.
Kakoso amefafanua kuwa bajeti ya Shilingi Trilioni 1.4 iliyopitishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2023/2024 haitoshelezi kukabiliana na matatizo yaliyopo katika miradi ya ujenzi wa barabara kwa nchi nzima.Kuna upungufu wa fedha za miradi ya maendeleo hasa katika ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja, barabara nyingi nchini ni mbovu na nyingine zimeisha muda wa matumizi na zinahitaji kujengwa upya ikiwemo barabara ya Dodoma – Iringa, Dodoma - Mwanza, Dar es Salaam – Mtwara na nyinginezo
Kakoso
Aidha, Kakoso amesema upungufu mkubwa wa fedha za matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja unaendelea kuiathiri sekta hiyo sambamba na kuwepo kwa mvua za masika zinazoendelea na kuathiri miundombinu, hivyo ni dhahiri kuwa fedha hizo bado hazitoshelezi.
0 Comments