RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano mkuu wa 79 wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM) unaotarajia kufanyika Mei 19 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Baraza hilo Meja Jenerali Francis Mbindi amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili kama njia ya kueneza amani duniani, huku tunu za baraza ikiwa ni kuhamasisha mshikamano, urafiki, heshima, usawa, uadilifu na ushupavu.
Amesema,Tanzania imepata heshima ya kuandaa mkutano huo kutokana na kukidhi vigezo ikiwemo kupatikana kwa huduma staki pamoja na amani na utulivu uliopo nchini.
Amesema, mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam una wanachama kutoka nchi 140 huku akisema nchi zote wanachama wanatarajiwa kushiriki ambapo mbali na kushiriki mkutano huo wajumbe watapata fursa ya kutembelea mnara wa kumbukumbu ya mashujaa walioipigania Tanzania, kutoa heshima na kuweka mashada ya maua kama ishara ya kuwaenzi mashujaa hao.
Meja Jenerali Mbindi amesema, ujio huo utakuwa na manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kulitangaza Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kutoa fursa kwa lugha adhimu ya Kiswahili kwani itakuwa ni miongoni mwa lugha tano zitakazotumika katika mkutano huo.
Vile vile amesema utatoa fursa ya kiuchumi ambapo wafanyabiashara mbalimbali watapata fursa ya kufanya biashara zao na hivyo kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Aidha amesema, kwa mara ya pili Tanzania inapata fursa ya kuandaa mkutano huo ambapo mara ya kwanza ni mwaka 1991 ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe walitembelea mbuga za wanyama na hivyo kutangaza utalii nchini na kuingiza kipato kupitia sekta hiyo.
0 Comments