SERIKALI kupitia Mamlaka ya Kudhibiti
Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata kilogramu 1,965, 340.52 milioni za aina
mbalimbali za dawa za kulevya huku watuhumiwa 10,522 nao wakikamatwa katika
kipindi cha Januari hadi Disemba 2023.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama amesema kuwa kati ya watuhumiwa hao wanaume ni 9,701 na wanawake ni 821.
Amesema, jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa huku ikielezwa kuwa kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilizokamatwa katika kipindi cha miaka 11.
Aidha, Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Mhagama
Kwa mujibu wa Mhagama, katika kuhakikisha jamii inapata uelewa juu ya tatizo la dawa za kulevya, Serikali imepanua wigo wa utoaji elimu kwa kuelekeza nguvu kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo ambapo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoa elimu ya dawa za kulevya na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa nchini ambapo sasa zitaitwa klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya
0 Comments