VIONGOZI wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi
wa Umma ya Burundi (ARMP), wamewasili nchini kwa ziara ya siku tano kwa lengo
la kujifunza utendaji wa Serikali ya Tanzania unavyoongeza ufanisi katika
usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mfumo wa
Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST).
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuupokea ugeni huo jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Tanzania (PPRA), Bw. Eliakim Maswi amesema ujio wa Mamlaka hiyo ni sehemu ya mashirikiano ya nchi za Afrika Mashariki katika kubadilishana ujuzi.
Ameeleza kuwa moja kati ya mambo yaliyoivutia Serikali ya Burundi ni pamoja na hatua ya Tanzania kujenga Mfumo wa NeST unaoongeza uwazi, uwajibikaji na ushindani wa haki ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana kwenye kila ununuzi wa umma.
Tunashirikiana katika maeneo mengi na tunajifunza kutoka kwa kila mmoja. Sisi tukienda Burundi tunajifunza kutoka kwao na wao wakija kwetu Tanzania wanajifunza hatua tunazopiga katika kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma, na hii ni sehemu ya maazimio ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Bw. Maswi.
Disemba mwaka jana tulikuwa na ugeni kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) unaosimamia miradi mikubwa ya kilimo nchini na pia kule Burundi. Tulipofanya wasilisho kuhusu Mfumo wa NeST waliona ni hatua kubwa na nzuri, na IFAD wanashirikiana na sisi kuhakikisha tunafanikisha na tunautumia
Aidha, amesema kuwa PPRA imewaonesha wageni hao baadhi ya miradi mikubwa iliyofanywa na Serikali ya Tanzania jijini Dodoma kupitia taratibu za ununuzi wa umma, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Mji wa Serikali wa Mtumba unaofahamika pia kama Jiji la Magufuli (Magufuli City).
Aliongeza kuwa viongozi hao wa Burundi wameelezwa pia kuhusu sheria mpya ya ununuzi wa umma ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliisaini mwaka jana. Amesema watapitishwa kwenye sheria hiyo kujifunza kuhusu maboresho yaliyofanyika ili na wao wapate uzoefu mzuri.
Vilevile, Bw. Maswi amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa nchi za Afrika Mashariki ziko kwenye mchakato wa makubaliano ya kuwa na sheria moja ya ununuzi wa umma.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa ARMP- Burundi, Bw. Nduwimana Cloude amesema wamevutiwa na hatua ya Serikali ya Tanzania kujenga Mfumo wa NeST kwa kutumia wataalam wake wa ndani, hivyo wamekuja kujifunza. Pia, amesema wameshangazwa na jinsi ambavyo Serikali imejenga miradi mikubwa waliyoiona kama Mji wa Serikali wa Mtumba na UDOM na wanapenda kujifunza namna Serikali ya Tanzania inavyofanikisha.
Tunashukuru PPRA Tanzania walivyotupokea, tumekuja hapa kujifunza mfumo wenu wa NeST ambao tunafahamu upo vizuri na sisi tutafaidika na ujuzi huu. Tunafurahi sana kwakua sisi sote ni mara ya kwanza kuja Dodoma na tayari tumeshuhudia kazi nzuri iliyofanywa na Serikali na wananchi
Nduwimana.
Kwa mujibu wa ratiba ya PPRA, wageni hao wameelekea mjini Iringa kwenye kambi ya wataalam wanaojenga Mfumo wa NeST.
|
0 Comments