MKURUGENZI Mtendaji wa
Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika amesema
hospitali hiyo imeandika historia ya kupona kwa watoto
watatu waliokuwa wakiugua ugonjwa wa Selimundu baada ya kupandikizwa
uloto Miezi michache iliyopita.
Dkt. Chandika ameyasema hayo leo Januari 30 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema miezi michache nyuma walitoa taarifa juu ya uwepo wa huduma hiyo ya upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa Selimundu katika hospitali hiyo ya benjamini Mkapa.
Ni muda mfupi sana tangu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyofika hapa na kuzindua hizi huduma za upandikizaji uloto baada ya hapo tukaanza kupokea wagonjwa hao na mpaka sasa tumetibu watatu ambao wamepona kabisa na wamerejea shule wanaendelea na masomo vizuri
Hii ni huduma ambayo haijawahi kutolewa Nchini isipokuwa hapa katika hospital ya Benjamini Mkapa, na tumeona matokeo mazuri, na tukiangalia Tanzania ni Nchi ya Nne inayoongoza kwa ugonjwa wa sikoseli, hivyo naamini kupitia huduma hii inayotolewa hapa tunaenda kupunguza ukubwa wa ugonjwa huu kwa kiwango kikubwa sana
Dkt. Chandika
Dkt. Chandika amesema huduma hiyo ya upandikizaji wa uloto kwa Mgonjwa wa Selimundu ni huduma ya msingi kwani inasaidia kukuza uchumi wa Taifa kwa kuwa na vijana wenye afya njema ya kuweza kufanya kazi.
Huduma hii inasaidia kuwa na vijana wenye afya njema uchumi wa taifa letu haulemewi kwani tunakuwa na nguvu kazi ya kutosha
Inapunguza pia gharama kubwa kwa Wazazi na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na huduma hii inatolewa bure kabisa hamna gharama yoyote, Rais wetu Dkt. Samia ameshatoa fedha kwaajili ya kuwapatia matibabu Wananchi wote wenye matatizo hayo
Chandika
Dkt. Chandika ameongezea kwa kuwahimiza wazazi wenye wagonjwa wa Sikoseli kuwa wasiwafiche watoto wao majumbani kwani huduma hiyo imeletwa kwaajili yao na ugonjwa huo unatibika na unapona kabisa.
Wazazi msiogope kuwaleta watoto kutibiwa huduma hii ni bure kabisa inatolewa, na ipo kwaajili tenu, ni watoe tu wasiwasi kuwa ukitibiwa unapona na hivi karibuni tunaenda kuwapandikiza wengine kama saba hivi ambao tumewapokea
Chandika
Nae mzazi wa mtoto Elisha John mwenye Selimundu Bwn. John Joseph amesema miaka 11 wamekuwa wakihangaika na mtoto huyo na mama wa mtoto ilimlazimu aache kufanya shughuli za kiuchumi na kushughulika na mtoto.
Amesema mpaka sasa mtoto anaishi kama watu wengine wanavyoishi na wala hana chakula maalum na ametoa wito kwa wazazi nchini kuwapeleka watoto hospitalini hapo kwaajili ya kupata huduma.
0 Comments