WAZIRI wa Katiba na Sheria Balozi Dk. Pindi Chana amesema bado kuna vitendo vya rushwa nchini hali inayosababisha utekelezaji wa miradi kusuasua. Kutokana na hali hiyo ameshauri ushirikiano baina ya wananchi na serikali ili kutokomeza suala hilo
Waziri Dk.Chana ameyasema hayo jijini hapa jana, wakati akizundua maadhimisho ya siku ya maadili na Haki za Binadamu Kitaifa mwaka huu.
Kutokana na uwepo wa vitendo vya rushwa husababisha serikali kushindwa kutekeleza jukumu lake la kuhudumia wananchi ipasavyo kwasababu fedha za kutekeleza miradi zinaliwa na watu wachache hivyo miradi kushindwa kutekelezwa au kutekelezwa chini ya kiwango
Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kudhibiti rushwa ambapo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alielekeza TAKUKURU kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kukabiliana na ubadhilifu.
Katika hatua nyingine Dk.Chana, amemshukuru Rais Dk.Samia kwa uongozi wake imara na kuweka miundombinu sahihi ya kusimamia haki za binadamu ikiwemo kuwepo kwa muhimili imara wa Bunge na Mahakama ambayo hutumika kutunga sheria za Nchi.
Ili Taifa lipate maendeleo lazima lizingatie utu, maadili na kuheshimu haki za binadamu kwa watu wote ambapo Rais Dk.Samia anayafanya hayo kwa vitendo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma TAKUKURU Joseph Mwaiswelo amesema, siku ya maadili na haki za binadamu kwa mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo ‘ZINGATIA MAADILI, UTU, UHURU NA HAKI KWA WATU WOTE KWA MAENDELEO ENDELEVU.’
Amesema maadhimisho hayo
yatahusisha shughuli kubwa nne ambazo ni uzinduzi, jukwaa la wadau wa juhudi dhidi
ya rushwa, wiki ya huduma kwa umma na kilele cha maadhimisho.
Katika hatua nyingine Mwaiswelo amesema maadhimisho hayo yameandaliwa na taasisi 10 ambazo ni ofisi ya Rais – Ikulu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Fedha; Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais - Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Amezitaja taasisi nyingine kuwa ni taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma na Tume ya Utumishi wa Umma.
Ushirikiano wa taasisi hizi katika kufanikisha maadhimisho haya lakini zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ni wa muhimu sana kwa Taifa maana unahakikisha kunakuwapo na uzingatiaji wa utu, haki za binadamu, usawa, maadili, uwajibikaji na kupinga vitendo vya rushwa.
Ni wazi kwa kuendelea kushirikiana tukiweka mbele maslahi ya Taifa na si ya kitaasisi na kushirikisha wadau wengine waliopo hapa leo na wasiokuwapo, kusudio la kuwa na maadhimisho haya kila mwaka litatimia.
0 Comments