MHE. Mary Chatanda, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ametoa pongezi kwa uongozi
wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke (TRRH) kwa juhudi zao za kusimamia na
kuboresha huduma za afya. Katika ziara yake ya leo katika hospitali hiyo, Mhe.
Chatanda ameelezea kufurahishwa kwake na maendeleo na ubora wa kazi inayofanywa
na wataalamu na uongozi wa hospitali.
Ameongeza kuwa ubora wa huduma unatokana na juhudi zinazofanywa na wafanyakazi wote kwa pamoja.
Ziara hiyo ilihusisha pia Naibu Mwenyekiti wa
UWT, Mhe. Zainab Shomari, pamoja na Katibu Mkuu wa UWT, Mhe. Jokate Mwegelo, na
viongozi wengine wa UWT. Walipata fursa ya kutembelea Wodi za kina mama
waliojifungua na wale wanaosubiri kujifungua, ambapo walishuhudia juhudi za
hospitali katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali
hiyo, Dkt. Joseph Kimaro, ameelezea mikakati mbalimbali inayofanywa na hospitali
kuboresha huduma za afya. Amesisitiza kuwa hospitali inaendelea kukua na
kueleza kuhusu ongezeko la idadi ya madaktari bingwa. Pia, ametangaza mpango ya
kuanzisha miradi kama vile wa usafishaji damu (Dialysis), ambao unatarajiwa
kukamilika kwa ushirikiano na mdau wao muhimu, TPA.
0 Comments