TAASISI ZA UMMA 109 ZAUNGANISHWA KATIKA MFUMO WA GovESB

📌RHODA SIMBA 

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema hadi sasa jumla ya Taasisi za Umma 109 zimeunganishwa katika mfumo wa GovESB na mifumo 117 imesajiliwa, huku akitaja  miongoni mwa taasisi hizo ni  mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), wakala wa leseni za biashara (BRELLA), Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na zinginezo.

Hilo ni katika utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika Taasisi za Umma inaunganishwa na kubadilishana taarifa.

Mhandisi Ndomba ameyasema hayo leo Disemba 22 jijini Dodoma  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa jitihada za mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali kwa kujenga mfumo mkuu wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GovESB).

Amesema kuwa pamoja na agizo la Rais, mfumo huo umetengenezwa kwa kuzingatia kifungu cha 48(2) cha sheria ya serikali mtandao Na.10 ya mwaka 2019 kinachoitaka mamlaka hiyo kuanzisha na kuendesha mfumo unaowezesha mifumo ya TEHAMA Serikalini kuwasiliana na kubadilishana taarifa.

GovESB ni mfumo wa Kieletroniki unaounganisha mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma iweze kusomana na kubadilishana taarifa kila inapohitajika

Ametaja lengo la Mfumo huo ni kuziwezesha taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali kwa usalama, kupunguza urudufu wa mifumo, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuokoa muda kwakuwa taarifa hupatikana kwa wakati.

Amefafanua kuwa kabla ya kuanza kwa mfumo wa GovESB kulikuwa na changamoto mbalimbali za ubadilishaji wa taarifa katika taasisi za umma, zikiwemo kutumia muda mrefu kupata taarifa kwani taasisi zililazimika kuwasilisha maombi ya kupata taarifa inazohitaji kwa njia ya barua katika taasisi husika.

Utaratibu huu wa barua ulichukua muda mrefu kupata taarifa hizo jambo lililochangia kupunguza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi

Changamoto nyingime ilikuwa ni utofauti wa utaratibu wa kupata taarifa kutoka taasisi moja hadi nyingine kwani kila taasisi inao Utaratibu wake wa ndani wa kupata na kutoa taarifa na wakati mwingine utaratibu hubadilika

Mhandisi Ndomba.

Mhandisi Ndomba amesema awali ili mifumo ya TEHAMA iweze kusomana ililazimika kuunganisha mfumo mmoja kuzungumza na mifumo mingine kila inapohitajika ambapo amesema uunganishwaji huo ulisababisha urudufu wa mifumo,kupungua kwa usalama,kupunguza ufanisi wa mifumo na kuongeza gharama za usimamizi na uendeshaji wa mifumo ya TEHAMA.

Kupitia GovESB changamoto hizo zimetatuliwa na sasa taasisi zote zinabadilishana taarifa kupitia mfumo huu hupata taarifa zinazohitajika kwa wakati na kwa usalama zaidi, vilevile mfumo huu umesaidia kuokoa muda wa kuwahudumia wananchi lakini pia hupunguza gharama za kutengeneza mifumo midogo midogo ya TEHEMA inayounganisha na mifumo ya taasisi nyingine

Mhandisi Ndomba.

Hata hivyo Mhandisi Ndomba amesema kuwa e-GA imeshirikiana na Taasisi nyingine za umma ikiwemo TRA,TPA na Wizara ya fedha katika kusanifu mfumo wa pamoja wa Kieletroniki wa uondoshaji wa shehena maeneo ya forodha (Tanzania Electronic Single Window System-TeSWS).



  

Post a Comment

0 Comments