Mwalimu Mkuu wa shule ya Wasioona Buigiri Jonathan Samson (kushoto) akiwa ofisini kwake akiwa na wageni waliomtembelea ofisini kwake.(Picha kwa msaada wa mtandao) |
📌JOYCE KASIKI
LICHA ya serikali kutatua changamoto ya
vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wasioona, lakini bado
kundi hilo linakabiliwa na changamoto ya vitabu mguso hasa kwa darasa la awali
,darasa la kwanza na darasa la pili.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mwalimu mkuu
wa shule ya Msingi ya wasioona Buigiri iliyopo katika wilaya ya Chamwino Mkoani
Dodoma Jonathan Samson amesema, kumekuwa na changamoto ya vitabu mguso shuleni
hapo na hivyo kuathiri ujifunzaji kwa wanafunzi hasa wa darasa la awali, darasa
la kwanza na darasa la pili huku akisema upungufu wa vitabu vya michoro mguso
kwa makundi hayo upo kwa asilimia 75.
Amesema, upungufu huo ni changamoto kwa watoto kujifunza kutokana na ujifunzaji wao unategemea sana katika kuvitambua vitu au herufi kwa kugusa/kupapasa.
Kama inavyofamika kwamba shule yetu pamoja na kuwa na wanafunzi wenye ulemavu wa aina nyingine, lakini pia wanafunzi walio wengi ni wale wasioona ambao kujifunza kwao ni kwa kugusa, kwa hiyo tunapokuwa na uhaba wa vitabu mguso hasa kwa wale ‘bigginers’ (wanafunzi wanaoanza shule) inakuwa changamoto kubwa sana katika ujifunzaji wao.
Mwalimu Samson
Aidha Samson ameiomba Serikali
kuwashirikisha watu wasioona kwa asilimia 100 kuanzia wakati wa uandaaji
wa michoro (vitabu vya michoro mguso ) na kuvifanyia majaribio ili
washirikiane katika kuitambua michoro katika vitabu pindi tu vinapoandaliwa kwa
lengo la kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji wa watoto.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali na
wadau wengine wa Elimu kusaidia katika kuhakikisha changamoto hiyo inapata
ufumbuzi hasa kwa mwaka ujao ambao serikali inaanza kutekeleza mtaala mpya.
Kwa upande wake Rehema John Mkazi wa
Buigiri ameishukuru Serikali kwa namna inavyoshughulikia masuala ya watoto
wenye ulemavu kwa kuhakikisha nao wanapata haki yao ya msingi ya kupata elimu
huku akiiomba iendelee kuhakikisha inayaangalia makundi ya watoto wenye ulemavu
na kushughulikia changamoto zao mapema kwani wengi wao wana uelewa wa
taratibu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chamwino Dkt. Semistatus Mashimba amesema katika kushughulikia changamoto
hiyo,Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ipo kwenye mazungumzo na wadau
mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu.
Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi
na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inayowalenga watoto wenye umri wa miaka sifuri
hadi minane kuhakikisha kundi hili linafikia ukuaji timilifu, uzoefu unaonyesha
kuwa watoto wenye ulemavu wamekuwa wakitengwa kupata huduma muhimu kwa ukuaji
wao.
Jema Chaula kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Seriakali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Malezi, Makuzi
na Maendeleo ya Awali ya Mtoto amesema, amelipokea na ataliwalisha eneo
husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
0 Comments