TANZANIA Bara kuna vijiji 12,318 ambapo hadi kufikia jana tarehe 23 Novemba 2023 vijiji 11,313 vimeunganishwa na umeme huku vijiji 1,005 vilivyosalia wakandarasi wapo kazini kukamilisha na kuwasha umeme.
Inatarajiwa kufikia Juni, 2024 vijiji vyote vitakuwa vimewashwa umeme kabla ya lengo kwa sababu ya serikali na wadau wa maendeleo kuwekeza nguvu zaidi katika uwezeshaji.
Aidha, mpaka sasa jumla ya vitongoji 28,659 vimefikiwa na umeme kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo nchini.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Jones Olotu wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kueleza utekelezaji wa majukumu ya REA katika ukumbi wa NSSSF-Ilala Jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Olotu amesema kuwa serikali kupitia REA ipo mbioni kuhakikisha kuwa vitongoji 36,101 vinafikiwa na umeme na kwamba serikali imekwisha andaa mipango madhubuti na kufikia mwaka 2030 vitongoji vyote vitakuwa vimefikiwa na umeme.
Kuhusu changamoto ambazo REA inakabiliana nazo amesema kuwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ikiwemo uharibifu wa nguzo kutokana na shughuli mbalimbali za wananchi katika maeneo ambayo wanachoma moto ovyo.
Hata hivyo Mhandisi Olotu ametoa wito kwa jamii kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele kuilinda miundombinu ya nishati ili iweze kuwanufaisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati mbadala na Jadidifu Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa kwa sasa serikali kupitia REA inatekeleza mradi wa kupeleka umeme katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa.
Amesema kuwa Mradi huo unajumuisha ujenzi wa mifumo midogo ya kusambaza umeme katika maeneo yenye vyanzo vya nishati jadidifu kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ambapo mikataba miwili ya mradi wa Ikondo-Matembwe Hydro Power ulisainiwa mwezi Februari 2023 na mkataba wa mradi wa Mwenga Hydro Power ulisainiwa mwezi Machi 2023.
Amesema kuwa miradi hiyo itaunganisha jumla ya wateja wa awali 2,168 katika vijiji 42 kwa gharama ya Shilingi 3.06 bilioni.
Aidha, amesema kuwa Serikali kupitia REA imewapata waendelezaji watatu (3) ambao ni Jumeme, Volt Africa na Green Leaf Technology wa miradi ya kusambaza umeme kwa kutumia nguvu ya jua, itakayotekelezwa katika visiwa 28 vilivyopo katika mikoa ya Kagera (8), Mwanza (13), Mara (3) na Lindi (4) na hivyo kuunganisha wateja 9,515 kwa gharama ya Shilingi 11.18 bilioni.
Wakala unakamilisha taratibu za kusaini mkataba na Kampuni ya Jumeme wakati Kampuni za Volti Africa na Green Leaf Technology zikikamilisha taratibu za kimazingira kabla ya kuendelea na hatua ya kusaini mikataba
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Ndg Deodatus Balile ameipongeza REA kwa kazi kubwa inayoifanya ya kusambaza umeme vijijini kwani hatua iliyofikia mpaka sasa ni kubwa ya kuungwa mkono.
Pongezi hizi siyo tu za kwenye jukwaa, kwa wale waliopata fursa ya kufika vijijini wakaona kinachoendelea hakuna sehemu utapita bila kuona nguzo imelala chini, hongereni sana kwa kazi mnayofanya REA
Balile.
Kadhalika, ameitaka REA kuhakikisha kuwa inaongeza fursa ya kukutana na wahariri mara kwa mara ili kutoa elimu kuhusu miradi inayotekelezwa na serikali kupitia REA jambo litakalorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi na jamii kwa ujumla wake.
0 Comments