SPIKA wa Bunge la Tanzania na Rais wa IPU Mhe. Dkt. Tulia
Ackson (Mb) amezindua rasmi Bunge Marathon litakalofanyika tarehe 13
April 2024 Dodoma.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Msekwa, Bungeni Dodoma ambapo Spika amesema kuwa hiyo itakuwa njia mojawapo ya kuleta juhudi za wadau na taasisi mbalimbali zinazofanya kazi na Bunge kwa pamoja, ili kuchangia kwa lengo hilo mahususi.
Kama nilivyodokeza hapo awali, uendeshaji wa Bunge Marathon utakua na tija ya kukusanya rasilimali fedha na mali zitakazoweza kutumika kuboresha huduma za kijamii, kama vile katika ujenzi wa madarasa au shule, vituo vya afya au ununuzi wa vifaa tiba n.k, na hivyo itakuwa njia mojawapo ya Bunge kusaidia juhudi za Serikali katika kuwasogezea karibu Wananchi huduma hizo za kijamii
Aidha amesema kuwa Utaratibu wa Bunge kushiriki katika kuiunga Serikali mkono katika masuala ya kuleta maendeleo, sio jambo jipya, kwani masuala kama haya yamekwisha kufanyika awali.
Mathalani wakati wa Bunge la Kumi na moja, kulikuwa na kampeni kubwa ya kutatua tatizo la upungufu madawati katika shule zetu, sisi kama Bunge tulitoa mchango wa takribani Tshs. Bilioni Sita ili kutengeneza madawati kwa ajili ya shule zetu
Vile vile, Bunge limeshiriki katika kutatua changamoto ya kupata elimu, kwa mtoto wa kike, ambapo lilichangisha fedha toka kwa wabunge na kwa wadau wengine, zilizowezesha kujenga shule ya Wasichana ya Bunge, iliyopo eneo la Kikombo, hapa Dodoma, inayodahili wanafunzi wa Kidato cha Tano katika michepuo ya Sayansi, ambao waliofanya vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha Nne, Shule hii iliyokabidhiwa kwa Serikali mnamo Juni 2021,"amesema Dkt.Tulia.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Naibu Spika Mhe. Mussa A. Zungu (Mb), Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Mhe. Festo Sanga, Wabunge na Wadau mbali mbali wa michezo
0 Comments