SIMBACHAWENE AKIRI RUSHWA BADO TATIZO NCHINI

 ðŸ“ŒJASMINE SHAMWEPU

IMEELEZWA kuwa bado kuna malalamiko mengi ya wanananchi katika ofisi za umma kuhusu vitendo vya rushwa hali inayosababisha wengi wao kushindwa kuzifikia Huduma wanazohitaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema hayo Leo  jijini Dodoma  alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU).

Waziri Simbachawene amesema bado yapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuwepo kwa rushwa katika taasisi mbalimbali hali ambayo inasababisha wananchi kukosa huduma ambazo wanazihitaji.

Bado suala la rushwa ndogondogo ni tatizo sana kwa wananchi wetu na huko ndiko yapo malalamiko mengi ya watu kutokana na rushwa hiyo kuwanyima fursa ya kupata huduma.

Huduma hizo ni pamoja na elimu ngazi za chini, kati hadi vyuo vikuu, lakini pia huduma za afya, kodi na leseni ambako kumewekwa utaratibu mgumu na ukilitimba katika utoaji wa huduma ili tuu watu watoe rushwa ndipo wahudumiwe

Simbachawene

Aidha, amesema kutokana na hali hiyo kila taasisi inatakiwa kutengeneza mkataba wa huduma kwa wateja na TAKUKURU iwe nao kama sehemu ya kufuatilia utekelezaji wake.

Tukitoka tuu hapa tukaenda pale hospitali ya rufani ya mkoa wa Dodoma General tukajificha mahali na kuangalia namna shughuli zinavyoendelea kama ni muhudumu au daktari atakuwa anatoa huduma bora tutaona na kama kuna muhudumu ambaye atakuwa hatoi huduma bora tutabaini hivyo hizi rushwa ndogondogo zinakera sana wananchi kuliko hata hizi za ubadhirifu wa mabilioni ambayo wao hawayaoni

Simbachawene

Hata hivyo amesema   TAKUKURU, inapaswa kuendeleza kushughulikia watu wote ambao watabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa nchini bila kuangalia hali zao.

Tuwashughulikie watu wote wanaojihusisha na rushwa nchini zipo rushwa zinaoekana kabla ya kukamilika kwa miradi lakini zipo ambazo zinaanza kuonekana baada ya miaka mitatu tangu kukamilika kwa mradi hivyo wahusika wote wanatakiwa kukamatwa na kuhojiwa hata kama watakuwa wamestaafu

Amesema hali hiyo itasaidia kukomesha tabia ambazo zimekuwa zikifanywa na watumishi wa umma kujihusisha na rushwa na kuhama kituo cha kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salum Rashid Hamduni amesema, mkutano huo ni wa siku tatu ambapo lengo lake ni kujadili mafaniko na changamoto kwa mwaka uliopita ili kuzipatia suluhu.

Hamduni, amesema katika kipindi cha mwaka uliopita taasisi hiyo, imeokoa kiasi cha Sh. bilioni 171.9 ambazo zingeingia mifukoni mwa watu kama TAKUKURU isingefanya oparesheni mbalimbali kwenye miradi ya umma.

Aidha amesema mkutano huo utatoka na maadhimio ambayo watakwenda kuyafanyia kazi ili kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vya rushwa katika sehemu mbalimbali nchini.

 


Post a Comment

0 Comments