KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Dodoma Bi. Pilli Mbaga amepongeza Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
katika Wilaya ya Kongwa Leo Novemba 14, 2023 ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya
ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM)
Wilayani humo.
Katika ziara hiyo kamati ya Siasa ya Mkoa imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Barabara ya kiwango cha Lami ya Mwalimu Nyerere yenye urefu wa Km 1 Kwa thamani ya Shilingi 487,199,000.00 kutoka mfuko wa Jimbo wa Barabara , Ujenzi wa Miundombinu katika Hospitali ya Wilaya wenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.64 unaohusisha Wodi tatu za wagonjwa na Jengo la mama na mtoto.
Miradi mingine ni ile ya Kisima cha Maji katika Kijiji Cha Laikala "B" wenye thamani ya Shilingi 780,566,436.64 Shule ya Msingi Moleti iliyojengwa kupitia mradi wa BOOST Kwa thamani ya Shilingi 318,800,000.00 na mradi wa Kuboresha umeme kwaajili ya kutatua kero ya umeme hafifu kwa Wilaya za Kongwa Mpwapwa na Gairo, unaohusisha ujenzi wa njia ya msongo wa Kilovoti 33 kutokea kituo kidogo cha Zuzu hadi Mbande wenye thamani ya Shilingi 5,104,849,344.90.
Aidha, katika miradi yote hiyo Kamati imetoa Pongezi za dhati na kutoa Rai kwa Wananchi kuendelea kuiamini Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani imedhamiria kutatua kero zinazowakabili Wananchi.
Akipongeza Mradi wa ujenzi wa Miundombinu katika Hospitali ya Wilaya Bi. Mbaga amewataka Madaktari na Wauguzi kuwa na kauli nzuri kwa Wagonjwa ili kutimiza dhamira nzuri ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi wake.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, pamoja na kushukuru jitihada za Serikali za kuwaletea Wananchi Maendeleo, pia ametoa wito kwa Serikali Kuboresha taratibu zake katika kuhudumia Wananchi ikiwemo kutenga Fedha zinazojitosheleza kutekeleza Miradi mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Aidha Mhe. Ndugai amesikitishwa na kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara hali inayopelekea kurudisha nyuma jitihada za Wananchi katika kujiletea Maendeleo kupitia viwanda mbalimbali vya uzalishaji.
TANESCO ni lazima Muende na nia aliyonayo Mhe Rais baadhi ya desturi zenu lazima zibadilike ili muepushe kero hizi kwa Wananchi
Mhe. Ndugai.
Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma imehusisha viongozi mbalimbali wa kisiasa wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya Mkoa na Wilaya, pamoja na Wakuu wa Divisheni na Vitengo (Wataalamu) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ambapo Dhamira ya ziara hiyo ni kukagua Miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia Fedha mbalimbali zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe.Samia Suluhu Hassan.
0 Comments