DODOMA YAZINDUA MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

 ðŸ“ŒMWANDISHI WETU

WAZIRI wa Habari na Mawasiliano Mhe. Nape Nnauye (MB), kwa kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo, leo Novemba Mosi 2023, amezindua mpango wa kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan inayoanzia Mkoa wa Dodoma hafla iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. 

Hafla hiyo iliyohusisha urushwaji wa matangazo mubashara, imehusisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma zipatazo nane ( Bahi, Chamwino, Chemba, Dodoma Jiji, Kondoa TC, Kondoa DC, Kongwa na Mpwapwa) kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwekezaji wa fedha za Serikali kwenye miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri hizo mbele ya waandishi wa Habari 

Akifungua Mpango huo, Waziri Mhe. Nnauye amezungumzia lengo la mpango pamoja na kutaja faida zake kwa Serikali na wananchi.

Programu hii imebebwa na kauli mbiu ya "Tumekusikia, Tumekufikia". Ikimaanisha Serikali imesikia kilio cha wananchi wake na sasa imewafikia ili kutatua changamoto zao. Programu itafanywa na Wakuu wa mikoa pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri wakielezea miradi mbalimbali iliyoanzishwa na Serikali kwa wananchi wao.

Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ambazo ni Kodi za wananchi. Faida za mpango huu ni kurahisisha Mawasiliano kati ya Serikali na wananchi hivyo, wananchi mnapofikiwa na watekelezaji wa mpango huu, toeni ushirikiano kwa kuelezea mazuri yanayofanywa na Serikali. Pia mpango huu utaelezea hatua tulizopiga kwenye maendeleo" Mhe. Nnauye.

Awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurungenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi, amesema mikoa yote nchini na Halmashauri zake imekua ikipokea fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo ni wakati sasa wananchi kufahamu kwa kina miradi inayotekelezwa kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ametoa taarifa za utekelezaji wa miradi kwa fedha za Serikali kwa Mkoa wa Dodoma.

Mhe. Rais amedhamiria kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa mkubwa kwa hadhi ya makao makuu kwa kutupatia fedha za kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile shilingi Bilioni 220 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje, Mhe. amepeleka fedha nyingi Vijijini ambazo zimegusa sekta mbalimbali kama Elimu, afya, maji, umeme n.k. Dodoma tumefanikiwa kujenga madarasa 1,462 yanayoweza kubeba wanafunzi 73,100 tumejenga shule mpya 124, tumetoa pikipiki 109 kwa Maafisa Elimu, tumejenga vyuo vya ufundi chini ya VETA na kuimarisha sekta ya Elimu

Mhe. Senyamule 

Ameongeza kuwa kwa upande wa sekta ya afya zimejengwa Hospitali 3, Zahanati 47, vituo vya afya 11, yamefanyika maboresho kwenye hospitali mbili za Wilaya hali ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya Mama na Mtoto vitokanavyo na uzazi. Kwa upande wa ajira, watumishi 628 wameajiriwa kwenye sekta ya afya ili kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi. 

Pia miradi mbalimbali ya umwagiliaji inatekelezwa kama mradi wa ujenzi wa Bwawa la Membe (Chamwino), Bwawa la Msagali (Mpwapwa) na mengine yanayoendelea kutekelezwa. Kwa upande wa Nishati ya umeme, kuna mpango wa kufikisha umeme kwenye Vijijini 822 vya Mkoa wa Dodoma.

Akifunga mkutano huo, Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema ni muhimu kuhakikisha mpango mkakati huu ulioanzishwa unakua endelevu ili wananchi waweze kufikishiwa taarifa za maendeleo yanayofanyika kwenye maeneo yao. Pia ameelezea Mradi mkubwa unaotekelezwa na Serikali kwenye sekta ya Elimu.

Miradi inayotekelezwa na Serikali ni mingi sana kuliko muda wa kuyaelezea, kupitia kampeni hii, Mikoa na Halmashauri zote zitakwenda kujipambanua juu ya miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao. Kwenye sekta ya Elimu kwa sasa, Serikali inashughulikia mradi wa kuboresha Elimu ya awali ya msingi unaogharimu kiasi cha Shilingi Trilioni 1.15 kwa kujenga madarasa ya awali 12,000, Maktaba, vifaa vya kisasa vya Tehama katika shule zaidi ya 800

Dkt. Dugange

Mpango wa kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita umeanzia kwenye mikoa minne (Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam na Pwani) na utaendelea kwa mikoa yote 26 na Halmashauri 104 za Tanzania Bara. Mpango huu utaongeza chachu ya Mawasiliano kati ya Serikali na wananchi juu ya matumizi sahihi ya fedha za kodi zao katika kuwaletea maendeleo.





 

Post a Comment

0 Comments