MTAKWIMU Mkuu
wa Serikali Dkt.Albina Chuwa ametoa rai kwa watakwimu wa Halmashauri,
Wizara, Idara na Taasisi za Umma kufanya kazi ya ziada kwa kuwapatia viongozi
wao takwimu sahihi ambazo zimepata kibali kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu pale
wanapowasilisha taarifa kwa wananchi au viongozi wa juu ili kuepuka upotoshaji
wa takwimu.
Ameyasema hayo leo Novemba 21, jijini Dodoma wakati wa hafla ya kilele cha maadhimisho ya 33 ya Takwimu Afrika 2023 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ikishirikiana na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika. ambapo hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya ofisi za Takwimu huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule.
Watakwimu, tufanye kazi ya ziada kwa kuwapatia viongozi wetu takwimu sahihi kwani wanaposimama mbele ya wananchi haipendezi kusikia kiongozi anataka takwimu ambazo sio sahihi. Tuhakikishe takwimu tunazowapatia viongozi wetu zimepata baraka kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu kwani pale ndipo unapata Takwimu sahihi unazoweza kuzitumia sehemu yoyote
Dkt. Chuwa
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa Takwimu bora ulimwenguni pia ameelezea umuhimu wa Takwimu kwa nchi za Afrika.
Tanzania inatoa takwimu bora zinazoaminika si Afrika tu bali Dunia kwa ujumla. Mwaka 2010 Serikali ilitekeleza mradi wa Mpango kabambe wa Takwimu uliotekelezwa hadi mwaka 2018 na ambao uliimarisha upatikanaji wa Takwimu bora nchini,
Nitoe Wito kwa Ofisi ya Mtakwimu msambaze taarifa kwenye Halmashauri zetu kwani Takwimu zinatakiwa kutumiwa kwenye kutafsiri mipango ya maendeleo kwa sekta zote. Takwimu zinasaidia nchi za Afrika kufahamu idadi ya rasilimali watu iliyopo na makundi yake
Mhe. Senyamule.
Hata hivyo, maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Kamisaa wa Sensa kwa upande wa Zanzibar Balozi Mohamed Ally Hamza ambaye amesema maadhimisho hayo yana lengo kuu la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu matumizi ya sensa pia ushirikishwaji wa jamii unasaidia kuongeza thamani ya Takwimu zetu.
Maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika hufanyika Novemba 21 kila mwaka yakiwa na lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya Takwimu katika mipango ya nchi za Afrika kwani Takwimu zinahitajika wakati wowote.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo "Uboreshaji wa mifumo ya ushirikiano wa kitakwimu ili kuharakisha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA): Mchango wa Takwimu Rasmi katika mageuzi ya kiuchumi na maendeleo endelevu ya Afrika".
0 Comments