MKUU wa Wilaya ya Dodoma Jabiri Shekimweri amesema Ofisi za Taifa za Takwimu barani Afrika zinatakiwa kuendelea kuzalisha Takwimu rasmi na zenye ubora na kuzisambaza kwa njia rafiki na za kuaminika kwa wakati ili kuwezesha Serikali na wadau kufanya maamuzi yanayohusu utekelezaji wa eneo huru la biashara barani afrika.
Shekimweri ameyasema hayo leo Novemba 20 jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika ambapo amesema kuwa wakati Ofisi hizo zikifanya hayo hazina budi kuboresha mifumo ya ushirikiano wa kitakwimu ili Takwimu ziweze kuwafikia wadau kwa urahisi na kwa usahihi kwa kuzingatia matumizi ya njia rahisi za usambazaji wa Takwimu husika.
Kwa kushirikiana na Ofisi za Takwimu za afrika zitakuwa zinatekeleza lengo namba 17 la malengo endelevu ya Dunia ambalo linahimiza ushirikiano katika kutekeleza malengo hayo ambayo Nchi za afrika zimeridhia utekelezaji wake
Shekimweri.
Aidha amesema kuwa Ofisi za Taifa za Takwimu barani Afrika zina wajibu mkubwa wa kusaidia Nchi kufanya maamuzi yanayohusu sera kuhusiana na eneo huru la biashara Afrika.
Shekimweri amesema Takwimu zinakuwa na maana pale ambapo zinatolewa taarifa kwani zinakwenda kukidhi mahitaji kwa usahihi na idadi husika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa shughuli za kitakwimu NBS Emilian Karugendo amesema kuwa matumizi ya Takwimu rasmi ndio msingi wa kila kitu katika maisha, katika mipango na katika kufuatilia programu mbalimbali na utekelezaji wake.
Amesema kuwa kongamano hilo ni kuelekea siku ya kilele cha maadhimisho hayo ambapo siku moja kabla ya maadhimisho huwa wanafanya kongamano na kuwaweka pamoja watu tofauti tofauti kwa lengo kuwa na mjadala wa kina unaolenga kujikita katika kaulimbiu hiyo na kuweza kuidadafua na kuona ni namna gani kama nchi wanaweza kuendana na kaulimbiu hiyo.
Kusanyiko la leo lina lenga kuwa na mjadala huu ambao unaongozwa na wabobezi katika mada zinazoendana na kauli ya mwaka huu, kwahiyo baada ya ya ufunguzi tutaingia katika majadiliano ya moja kwa moja na tutakuwa na mada mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa mifumo ya ushirikiano wa kitakwimu ili kuharakisha utekelezaji wa eneo huru la biashara la Afrika (AFCFTA) mchango wa Takwimu rasmi na 'big data' katika mageuzi ya kiuchumi na maendeleo endelevu ya afrika,
Mada nyingine ni matokeo ya sensa ya watu na makazi mwaka 2022 na mwongozo wa kitaifa wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yanawezaje kutumika kwa pamoja na matokeo ya tafiti nyingine ili kuongeza matumizi na thamani ya Takwimu rasmi katika sekta ya kilimo nchini?,"amesema.
Kwa upande wake Godfrey Saga Mhadhiri Chuo Cha Takwimu Mashariki mwa Afrika amesema kuwa lengo kubwa la kongamano hilo ni kuweka ufahamu katika tasnia hiyo ya Takwimu kuanzia shughuli za ufundishaji masuala ya utafiti na masuala ya ushauri wa kitaalamu pamoja na kutumia taarifa hizo zinazotokana na takwimu mbalimbali.
Tunawashukuru sana Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuungana na chuo cha Takwimu ili kuweza kulisukuma hilo gurudumu la kuisaidia Serikali katika kueneza habari ya Takwimu sababu mipango mbalimbali ya Nchi haiwezekani bila kuwa na Takwimu rasmi
Maadhimisho hayo yamebebwa na kauli mbiu isemayo "Uboreshaji wa mifumo ya ushirikiano wa kitakwimu ili kuharakisha utekelezaji wa eneo huru la biashara la Afrika (AFCFTA) mchango wa Takwimu rasmi na'big data' katika mageuzi ya kiuchumi na maendeleo endelevu ya Afrika.
0 Comments