📌MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Global Green Growth (GGGI) Dkt. Frank Rijsberman jijini Seoul nchini Korea Kusini.
Katika mazungumzo yao pamoja na mambo mbalimbali wamejadiliana kuhusu utayari wa nchi kuwa mwanachama wa GGGI na kushirikiana na taasisi hiyo kuijengea uwezo Tanzania katika kuandaa programu, miradi na mikakati ya kufaidika na fedha na uwekezaji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (climate financing).
Aidha, Waziri Dkt. Jafo ameshiriki Mkutano Mkuu wa 12 na Kikao cha 16 cha Baraza la Nchi Wanachama wa Taasisi ya Kimataifa ya Green Global Growth wenye kujadili masuala mbalimbali kuhusu hifadhi ya mazingira.
Taasisi hiyo ya kimataifa yenye makao makuu yake katika Jiji la Seoul nchini Korea Kusini, ina takriban wanachama 48 na kati yao sita wanatoka katika Bara la Afrika Afrika.
Katika hatua nyingine akiwa katika ziara hiyo ya kikazi, Waziri Mhe. Dkt. Jafo amepata nafasi ya kushiriki katika mkutano na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini.
Mjadala katika mkutano huo mada iliyoandaliwa ni fursa zilizopo katika nchi hiyo za mazingira ambazo Tanzania inaweza kunufaika nazo zikiwemo Biashara ya Kaboni (Carbon Credit), Uchumi wa Buluu (Blue Economy) na Udhibiti wa Taka (Waste Management).
Waziri Jafo yupo ziarani nchini Korea Kusini kwa ziara ya kikazi ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha ushirikiano katika masuala ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo ni matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akiimarisha diplomasia na mataifa mbalimbali duniani.
0 Comments