WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo
amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza wigo
wa kuandaa miongozo ya tathimini ya athari za mazingira (TAM) kupitia sekta za
viwanda, nishati, kilimo na maji ili kuharakisha zoezi la mapitio ya miradi ya
tathimini za athari kwa mazingira.
Akizungumza
jana Jumatano (Oktoba 18, 2023) Jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa ukaguzi wa mazingira kwa miradi ya
ujenzi wa majengo ulioandaliwa na NEMC kwa kushirikiana na Kituo cha Sayansi na
Mazingira cha Nchini India (CSE), Dkt. Jafo amesema uhifadhi na usimamizi
wa mazingira ni mojawapo ya maeneo ya vipaumbele vilivyopo katika malengo makuu
ya Serikali.
Dkt. Jafo amesema mwongozo ambao umezingatia
mahitaji halisi ya nchi ikiwemo ukuaji wa miji na majiji, limeipa NEMC mamlaka ya kuhakikisha hali ya
mazingira inaboreshwa nchini kwa kusaidia uboreshaji wa afya ya jamii ikiwa ni
pamoja na mazingira vinalindwa na kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini.
Kipengele Na. 17 cha Makubaliano ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu unazitaka nchi wanachama kuhusisha tathmini za athari za mazingira katika miradi ambayo inasababisha madhara kimazingira katika kutekeleza kipengele hicho zilianzisha taasisi, na kutengeneza Sera na Sheria ikiwa ni pamoja na Kanuni kama ilivyo kwenye Kanuni ya Athari ya Mazingira za Mwaka 2005 na zile za Mwaka 2018
Dkt. Jafo.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Tathmini za Athari kwa Mazingira
(TAM) hufanyika ili kuweka mifumo bora ya kulinda mazingira ikiwa ni pamoja na
kupunguza kiwango cha taka zinazozalishwa, kutoa kipaumbele katika masuala ya
jamii, kuainisha athari zilizopo na madhara yanayoweza jitokeza kutokana na
miradi inayoanzishwa.
Waziri Jafo amesema NEMC inapokea zaidi ya miradi 2000
kwa mwaka kwa ajili ya mapitio na kuongeza kuwa idadi hiyo ya miradi ni kubwa
na itaweza kupitiwa kwa ufanisi iwapo kutakuwa na miongozo ya kila sekta kama
inavyoelekezwa katika Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
Dkt. Jafo ameishukuru Serikali ya India kupitia
kituo hicho kwa kushirikiana na NEMC katika kuandaa mwongozo huo kwani
ushirikiano huo ni ishara ya matokeo ya ushirikiano wa taasisi hizo katika
kupatia ufumbuzi wa changamoto za kimazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sayansi na
Mazingira cha Nchini India (CSE), Nivit Yadav amesema Tanzania ni nchi ya tatu
Bara la Afrika yenye kasi kubwa ya idadi ya watu na nchi ya pili kwa Mataifa ya
Afrika Mashariki kuwa na kasi ya ukuaji wa sekta ya ujenzi, hivyo suala la
tathmini ya miradi ya ujenzi ni jambo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele
katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Amesema Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira
ya mwaka 2004 imeanisha vipaumbele mbalimbali vya utekelezaji wa Sheria hiyo
ikiwemo kanuni na miongozo ya utekelezaji ikiwemo ushirikiano baina ya Serikali
w ikiwemo NEMC na CSE.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi
na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka amesema kwa muda mrefu
kumekuwepo na changamoto ya usimamizi wa tathmini ya athari kwa mazingira
kupitia maandiko ya miradi mbalimbali yanayowasilishwa kwa ajili ya utoaji wa
vibali vya mazingira.
Awali wataalamu wetu hawakuwa na mwongozo wa maandiko ya tathmini ya miradi ya athari za mazingira ambayo inakidhi matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kanuni zake….Baada ya uzinduzi huu sasa wataalamu elekezi wa mazingira na wadau watakuwa na mwongozo wa uaandaji wa maandiko kwa kuzingatia viwango na ubora unaohitajika
Dkt. Gwamaka.
0 Comments