WANANCHI MITAA YA ZEPISA A NA B WAIANGUKIA SERIKALI KUPATA HUDUMA ZA MAJI, UMEME NA BARABARA

 ðŸ“ŒMWANDISHI WETU

WANANCHI wa Mitaa ya Zepisa A na B kata ya Hombolo, Jijini Dodoma wameiomba serikali kuwatatulia matatizo yao wanayodai yanawatesa kijijini hapo kwa muda mrefu toka mwaka 1972  bila barabara ya kueleweka, maji wala umeme.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kufikisha ujumbe wao kwa serikali, wananchi hao wameomba kufikishiwa huduma hizo muhimu kwa wakati

Pendo Wilson ni mwananchi wa mtaa wa Zepisa B alisema wanawake ndiyo wanaoteseka zaidi hasa wanapoumwa uchungu kwani kituo cha afya kipo mbali halafu barabara siyo nzuri imejaa mchanga kupita na pikipiki ni hatari kwa afya zao.

Mmeona mlikopita pale sisi ndo tunapita kwenda kujifungua tunadondokea pale kwenye lile daraja na lile daraja lilikuwa ndani ya barabara lakini sasa hivi limetengana barabara ipo sehemu nyingine na daraja sehemu nyingine na imejaa mchanga

Pendo.

Kwenye maisha kila kitu ni maji lakini siyo kwetu sisi tunaishi maisha magumu sana kwenye suala la maji tunatembea usiku kutafuta maji ni mateso, serikali tusaidieni hali ni mbaya

Ernest Mchuno mkazi wa mtaa wa Zepisa A, alisema kuwa wamekuwa wakilalamika kwa viongozi mbalimbali wanaokuja mtaani hapo kila mara kuhusu huduma hizo zinavyowatesa bila mafanikio kwa muda mrefu.

Waandishi tunaseka hadi tunajiuliza tumemkosea nini Mungu,viongozi wa serikali wanakuja huku na magari yao mazuri mengi lakini hawafanyi chochote nyie wenyewe mashahidi mmeona barabara ile inawatesa wake zetu wakati wa kujifungua hadi kufika hospitali ile mlioina kule, cha kushangaza hapa wametujengea kituo cha afya ambacho hakina maji, sehemu ya kuchomea taka hakuna, hata choo hakuna na umeme pia hakuna, mtu akiumwa usiku hakuna pa kwenda jamani tunateseka.

Naye Mzee  Emily Makasi alisema "Pamoja na waliyozungumza wenzangu lakini suala la maji ni shida sana wanawake zetu wanaenda kwenye maji saa sita usiku wanarudi saa nne asubuhi kwajili ya kisima kimoja cha maji na hayatoki kama inavyotakiwa tunayasubiria na foleni ni kubwa."

Alisema licha ya kuwa na vyoo vizuri katika shule wanayosoma watoto wa mitaa hiyo lakini wanaenda chooni bila maji huku vyoo walivyojengewa na wafadhili  vinatakiwa kutumia maji mengi lakini hakuna maji hata kidogo hivyo  kupelekea kuwa na wasiwasi ya magonjwa ya mlipuko kwani hali ya vyoo hivyo ni mbaya na ukiangalia watoto wanaingia bila hata ya viatu.

Huku hata walimu wanaletwa lakini wakiangalia mazingira wanaondoka, hakuna umeme wala maji na kila mara tumekuwa tukilalamika kwa viongozi wetu wa mitaa wanafuatilia lakini hakuna majibu ya kueleweka na hadi leo tunateseka halafu tupo ndani ya jiji

Mzee Makasi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Zepisa B , Mussa Rashid akiongelea changamoto hizo katika mtaa wake alisema kweli limekuwa tatizo kubwa kwenye mtaa wake na kuwa matatizo hayo yamekuwa yakiwagombanisha wao na wananchi wao kwani wakiwaita kwenye mikutano wananchi hawaji kwasababu wanaona wanaenda kuongelea mambo yale yale yasiyotekelezeka.

Huku Mwenyekiti wa Mtaa wa Zepisa  A, Daudi Kamunya, akisema kuwa kweli changamoto hizo zipo na wao kama viongozi wa mitaa wamefutilia sana bila mafanikio lakini yeye hajakata tamaa kwani ataendelea kufuatilia kwani wananchi wanataka maendeleo na maendeleo ni huduma za kijamii kama hizo ambazo bado hawajazipata.

Nawasihi wananchi wawe wavumilivu tunaendelea kuiomba Serikali itusaidie hizi huduma ni za lazima ndiyo maana hadi leo tunaendelea kuzilalamikia

Kamunya.




 

 

Post a Comment

0 Comments