OFISI YA MAKAMU WA RAIS YATOA SEMINA UCHUMI WA BULUU

📌MWANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kutunga Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu na Mkakati wake wa utekelezaji kwa lengo la kuweka mfumo jumuishi wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali zake ili kukuza uchumi wa nchi na maendeleo endelevu.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi wakati wa Ufunguzi wa Semina ya Uchumi wa Buluu na Mabadiliko ya Tabianchikwa Wizara za kisekta leo Oktoba 17, 2023 jijini Dodoma.

AmesemaUchumi wa Buluu ni dhana ambayo inachagiza ukuaji wa uchumi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali maji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii.

Bw. Mitawi amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo washiriki kuhusu jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia programu ya Msaada wa Kibajeti pamoja na Kukuza na kuongeza ujuzi katika masuala ya  uchumi wa buluu na mabadiliko ya tabianchi.

Sote tunatambua kwamba mabadiliko ya tabianchi yapo na ni ya kweli na tayari athari zake zimeshaanza kuonekana na zimeleta madhara makubwa katika maeneo ya bahari na mito nchini kama  tunavyoshuhudia vimbunga, El-Nino pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari na mito amesema Mitawi.

Hivyo, kwa muktadha huo ametoa wito wa kuchukua kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kulinda na kuhifadhi Misitu yetu, vyanzo vya maji na rasilimali zote ambazo ndio tegemeo katika nyanja ya Uchumi wa Buluu.

Aidha, ameishukuru Jumuia ya Ulaya kwa kusaidia Serikali kutekeleza shughuli zenye mnasaba na uchumi wa buluu ili kujenga uchumi imara na endelevu kupitia shughuli  za uchumi wa buluu.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa amesema semina hiyo ya siku mbili mbali ya kuwashirikisha wataalamu kutoka Tanzania Bara pia itawafikia Tanzania Zanzibar.

Amesema masuala ya mabadiliko ya tabianchi ni eneo lenye changamoto hivyo Tanzania imekuwa na programu mbalimbali inazotekeleza kama nchi mwanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Ameongeza kuwa kwa sasa Tanzania inajiandaa kushiriki katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaotarajiwa kufanyika Dubai, Falme za Kiarabu hivi karibuni ambapo masuala ya uchumi wa buluu yatakuwa ni kaulimbiu ya kitaifa





Post a Comment

0 Comments