KATIBU MKUU YONAZI AWATAKA SUMA JKT KUONGEZA KASI UJENZI JENGO LA OFISI YA MAKAMU WA RAIS

📌MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya SUMA JKT imetakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo Ofisi ya Makamu wa Rais unaoendelea katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya jengo hilo  Oktoba 23, 2023.

Dkt. Yonazi ameiomba Ofisi ya Makamu wa Rais kusimamia kwa ukaribu ujenzi huo ili jengo hilo liweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora kuwawezesha watumishi kulitumia.

Tuna imani na SUMA JKT lazima tuoneshe hata kampuni za ndani hasa hizi za umma zina uwezo wa kujenga na hatutegemei kuona mnafanya kazi ambayo hairidhishi, tunataka kuona kazi nzuri tiles  zimenyooka, rangi imekaa mahali pake

Aidha, Katibu Mkuu huyo amehimiza usalama mahali pa kazi kwa wafanyakazi wanaojenga majengo hayo ikiwemo kupewa vifaa na elimu ya kujilinda dhidi ya majanga yanayoweza kutokea wakati wanaendelea na kazi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo uko nyuma kwa takriban siku 83.

Mitawi amefafanua kuwa kutokana na uchelewaji huo, mshitiri ambaye ni Ofisi ya Makamu wa Rais iliwaelekeza wawasilishe mpango kazi wa namna gani wanaweza kuzifidia siku hizo zilizopotea.

Hata hivyo amesema wataendelea kuwasimamia kwa ukaribu kuhakikisha kazi ya ujenzi wa jengo hilo lenye thamani ya shilingi bilioni 18.8 inakamilika kwa ubora unaotakiwa.

Mkataba wa ujenzi wa jengo hilo chini ya Msimamizi Elekezi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ulisainiwa Oktoba 13, 2021 jijini Dodoma huku ukitarajiwa kukamilika Novemba 2023.


  

Post a Comment

0 Comments