JAMII imeshauriwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ili kufanikisha kampeni ya "Tokomeza rushwa na dawa za kulevya shuleni na vyuoni" ili kujenga Tanzania isiyokuwa na rushwa wala dawa ya kulevya.
Hayo yamesemwa Oktoba 4 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) CP Salum Hamduni wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanywa pamoja na Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) CG Aretas Lyimo.
CP Hamduni amesema matarajio ya kampeni hiyo ikitekelezwa kwa ushirikiano na wadau wote nchini ikiwemo waandishi wa habari na wadau wote hususani katika ngazi ya elimu utafikia lengo la udhibiti wa vitendo hivyo.
Tukizungumzia shuleni na vyuoni itachangia katika kuongeza uelewa kwa wanafunzi, vijana, na jamii kwa ujumla kuhusu ukubwa wa tatizo la rushwa na madhara ya dawa za kulevya katika jamii yetu
CP Hamduni
Naye Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) CG Aretas Lyimo amesema kupitia kampeni hiyo iliyozinduliwa ikienda kukamilika malengo ya serikali yanaenda kutimia.
Tunaamini kwamba elimu hii ikifikia makundi haya Tanzania inaenda kuwa salama na malengo ya kiuchumi yanaenda kukamilika kwani kupitia wanafunzi na vyombo vya habari jamii itapata elimu ya kuwa na maadili na kuwa wazalendo wa nchi yao katika kujenga taifa na liweze kukua vizazi na vizazi
CG Lyimo
Kampeni hiyo inalenga kutokomeza rushwa na dawa za kulevya kupitia klabu za wapinga rushwa na dawa za kulevya mashuleni na vyuoni kwa nchi nzima ambapo matarajio hasa ya kampeni hiyo ni kuwafikia vijana ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa elimu.
0 Comments