MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philp Isdori Mpango ameyataka mashirika yasiyo ya Kiserikali kuzingatia maadili ya utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kuwa wawazi kwa rasilimali zote wanazopata kwa maslahi ya Taifa.
Ameyasema hayo leo Oktoba 5 jijini Dodoma wakati akifunga jukwaa la mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambapo amesema NGOs zote zinapaswa kuzingatia na kutunza maadili ya kitanzania katika utekelezaji wa miradi yao.
NGO's msikubali kutumiwa kinyume na sheria, maadili na mila zetu, msikubali kutumiwa na watu wasiotutakia mema wakiwa na nia mbaya ya kuharibu
Dkt. Mpango
Amesema Serikali inaahidi kuendelea na jitihada za kuondoa baadhi ya changamoto zinazoathiri ufanisi wa NGOs nchini na kuzitaka NGOs kuwa na uwazi jinsi ya uendeshaji wa shughuli zao.
Watendaji wa Serikali msiwe kimya mnapoandikiwa barua na NGOs, zinatakiwa kujibiwa ili wapate majibu kwa lengo husika, NGOs andikeni changamoto zote za kikodi na kuzipeleka Wizara ya Fedha, zitafanyiwa kazi
Dkt.Mpango
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara kupitia msajili wa NGOs ina jukumu la kusajili na kuratibu shughuli za mashirika haya ili kuhakikisha zinaleta tija katika jamii kwani zimekuwa zikiunga mkono jitihada za Serikali kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali zinazowagusa wananchi.Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya utendaji kazi ikiwemo kuanzisha madawati ya uratibu wa NGOs katika sekta mbalimbali
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Dkt. Lilian Badi amesema Sekta ya mashirika yasiyo ya Kiserikali inaendelea kukua mwaka hadi mwaka siyo tu kwa idadi inavyoongezeka bali utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, mazingira, ulinzi wa jamii, uwezeshaji wa wananchi, elimu, kilimo, jinsia, maji, utawala bora na haki za binadamu.
Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya mashirika yasiyo ya Kiserikali ili kutekeleza majukumu yetu kwa ajili ya maslahi ya Watanzania na Taifa kwa ujumla
Badi
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Serikali, Bi. Mwantumu Mahiza amesema wana jumla ya NGOs takribani 10,000 ndani ya nchi, ambapo mashirika hayo yanafanya kazi ya kujitolea kwenye jamii, hivyo yanahitaji kushikwa mkono na Serikali.
Tunaomba Makamu wa Rais uzielekeze mamlaka za mikoa na wilaya kufanya kazi kwa karibu sana na mashirika haya ili kazi ya kujenga Taifa isonge mbele
Mwantumu
0 Comments