RUWASA DODOMA KUPELEKA MAJI KATIKA VIJIJI 177

 ðŸ“ŒRUCIANA  NYONI

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mzingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Dodoma, imesema katika mwaka huu wa fedha imeweka kipaumbele kuvifikia Vijiji 177 ambavyo havina huduma ya maji ili kuwapunguzia wananchi  adha  ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Hayo yamebainishwa jijini hapa jana na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Mbaraka Ally wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa taasisi hiyo kwa mwaka huu wa fedha .

Amesema kwasasa  RUWASA inahudumia vijiji 693  ambapo kati ya vijiji hivyo  565  vimefikiwa na huduma ya maji  na viijiji 177 bado havijafikiwa  na huduma hiyo.

Mikakati iliyopo katika mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha vijiji 177 ambavyo havina huduma ya maji vinawekewa kipaumbele cha kwanza kupeleka miradi ili wananchi wa maeneo husika waanze kupata huduma ya  maji 

Katika hatua nyingine Mhandisi Ally amesema katika mwaka wa fedha ulioisha RUWASA Dodoma kulikuwa na miradi ya maji 62 ambayo mingi ipo katika hatua za ukamilishaji na  inaendelea kutekelezwa.

Amefafanua kuwa kadri miradi ya maji inavyoendelea kutekelezwa inaongeza asilimia za upatikanaji wa maji hivyo na kupunguza idadi ya vijiji ambavyo havina huduma hiyo muhimu.

Tunaendelea kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025 ambayo imeelekeza huduma ya maji kwa wananchi wa vijijini ifikie asilimia 85. Tuna imani hadi kufikia muda huo tutatekeleza kwasababu hadi sasa hali ya upatikanaji maji kwa vijiji vya Mkoa wa Dodoma imefikia asilimia 65

Mhandisi Ally ameongeza kuwa, katika mwaka  huu wa fedha serikali imeitengea RUWASA sh.bilioni 17 kwa ajili kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji

Kwa mujibu wa Meneja huyo amebainisha kuwa kwasasa wilaya inayosumbua kwa upatikanaji wa maji ni Bahi, Kondoa  na Chemba  hivyo wamejipanga kuhakikisha miradi yote inatekelezwa ili kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma hii muhimu.

Mhandisi Ally amesema RUWASA inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati katika wilaya zote ili kuhakikisha inatoa maji kwa uhakikika na kuhudumia vijiji vingi zaidi.

Tunafanya kazi tunahakikisha huduma ya maji mkoa wa Dodoma inaimarika na wananchi wanapata huduma hiyo pasipo kikwazo chochote ili kuerndelea kuunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani

 

Post a Comment

0 Comments