ZILIKUWA nyakati ngumu kwa Sir. Alex
Ferguson wakati akiwaza mrithi wa Roy Keane ambaye alikuwa mchezaji mtata na
mwenye makeke mengi kwenye dimba la kati la Manchester United.
Katika mchakato wa kumpata kiungo
mkabaji halisi alijikuta akimsajili Sebastian Veron lakini alishindwa
kumshawishi na kumuuza Chelsea na yale mawazo yakaendelea kuisumbua akili yake.
Wakati wa michuano mikubwa ya Africa Cup
Of Nations ya mwaka 2003 jicho la mpelelezi wa Ferguson lilitupia ndoano katika
talanta za waafrika hatimae likainasa sura ya gwiji la Kamerun. Unamjua ni
nani?
Alikuwa Eric- Daniel Djemba Djemba Kiungo
mkabaji mwenye uwezo mkubwa wa kutembea na mpira eneo la kati, Djemba
aliituliza akili ya Sir Alex Ferguson kwa ule uwezo wake. Wakati huo alikuwa
akiitumikia Nantes ya nchini Ufaransa.
Ferguson bila kupepesa macho aliweza
kumsajili Eric Djemba wakati huo Roy Keane akielekea ukingoni mwa soka lake, zilikuwa
zama za Cristiano Dos Santos Ronaldo na kipaji chake bado unaongezewa Eric Djemba
na mpira wake.
Kumhusudu sana kijana wake Ferguson
akampa mshahara mkubwa Djemba ili kuipandisha thamani na morali ndani ya klabu,
ila kilichotokea Djemba aligeuka kuwa mtu wa starehe, kila mwisho wa wiki
akipokea mshahara kijana huyo alikuwa anashusha gari mpya na kukesha katika
kumbi za starehe kitu ambacho kilimfanya kuwa na wakati mgumu kupata namba
kikosini.
Tukio lile lilimkera sana Ferguson na
kusema tatizo lilikuwa kumpa Djemba mshahara mkubwa,
alidhani anamjenga kumbe anabomoa maisha yake. Baadae alimuuza katika klabu ya
Aston Villa sehemu ambayo hakudumu na kuishia kutimkia Burnley kwa mkopo wa
miezi sita kisha kufungasha virago na kukimbilia Qatar.
Huyo ndiyo
Djemba Mkameruni wa kwanza kucheza Manchester United, Onana ameweka rekodi ya
kuwa mchezaji wa pili na golikipa wa kwanza kutokea bara la Afrika kuidakia
United. Amesajiliwa na kocha Eric Ten Hag kwa kitita cha Euro 47.2 milioni
ikikadiliwa kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 148 za Kitanzania akitokea katika
klabu ya Inter Milan iliyo na masikani yake jiji la Milan nchini Italia.
Kipa huyo anapaswa kuikwepa kasumba ya
Eric Djemba na kuendeleza kipaji chake, Djemba baadae alisema anayajutia sana
maisha ya jiji la Manchester, kwakua ni kijana masikini aliyeishi kitajiri
katika jiji maarufu na la gharama na hatimaye kuendekeza starehe na kukatiza
kipaji pamoja na ndoto zake.
0 Comments