BALOZI wa Indonesia nchini Tanzania Bw. Tri Yogo
Jatmiko pamoja na ujumbe wake, wamemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Rosemary Senyamule ofisini kwake leo Septemba 19 kuzungumza kuhusu utaratibu wa
kuhamishia ofisi za Ubalozi huo kwenye Mji Mkuu wa Serikali Dodoma kwa lengo la
kutekeleza agizo la Serikali la kuhamishia Makao Makuu ya nchi Mkoani Dodoma na
kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika mazungumzo yao Balozi Jatmiko amesema
mwezi uliopita Rais wa Indonesia alikuja Tanzania na kuonana na Mhe. Rais Samia
ambapo moja ya mambo waliyozungumza kubwa lilikua ni swali kutoka kwaMhe. Rais
Samia kuhusu lini Ubalozi wao utahamia Dodoma. Kufuatia mazungumzo ya viongozi
hao, Mhe. Balozi ameamua kufunga safari hadi kwenye ofisi hii ili kupata utaratibu
wa ujenzi wa ofisi za Ubalozi kutoka kwa mwenyeji wao Mhe. Senyamule.
Akitoa ufafanuzi juu ya eneo lililotengwa kwaajili
ya Mabalozi wa nchi mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba, Mratibu wa Mradi
wa ujenzi wa Mjiwa Serikali Dodoma Bw. Meshack Bandawe, amesema kuwa Balozi zote
zilizopo nchini zimetengewa maeneo maalumu na yenye ukubwa unaolingana wa heka
2.5 kwa eneo la ofisi na pia kuna maeneo kwaajili ya makazi na watumishi wa Balozi
hizo. Amewaonyesha ramani ya eneo lao ikiwemo majirani waliopakana nao ambao ni
Ubalozi wa Burundi, Algeria, Namibia pamoja na Vietnam. Hata hivyo, amebainisha
kuwa ujenzi wa Mji wa Serikali kwa sasa umefikia asilimia 70 hadi 80.
Balozi Jitmiko amesisitiza kupatiwa nyaraka zitakazohusiana na eneo lao ili aweze kuziwasilisha kwa Waziri wao na kujadiliwa kwenye Bunge la Indonesia kwa ajili ya kupangwa bajeti ya ujenzi ili uweze kuanza mara moja. Pia Balozi huyo amesema Indonesia ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya kiteknolojia ikiwemo kwenye sekta za madini na umeme kwani huko kwao Wana teknolojia za kisasa.
0 Comments