📌RHODA SIMBA
TUME ya Madini imesema kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanikiwa kuanzisha jumla ya masoko ya madini 42 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 94 nchini.
Hayo yameelezwa leo Agosti 18 jijini Dodoma na Kaimu katibu Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo Ramadhan Lwamo wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha mwaka 2022/23 na mikakati ya mwaka 2023/24.
Amesema kuwa uanzishwaji wa masoko hayo ulianza rasmi tarehe 17 March 2019 kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa biashara ya madini nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini kwa Serikali.
Kwa mwaka wa fedha 2022/23 masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilichangia jumla ya shilingi 157,428,350.41 kama mrahaba na ada ya ukaguzi wa madini nchini sawa na asilimia 23.22 ya makusanyo yote yaliyokusanywa na Tume kwa mwaka husika
Kadhalika amesema kuwa katika kuendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta ya madini nchini katika mwaka wa fedha 2022/23, tume ilifanikiwa kutoa jumla ya leseni 9,642 kati ya leseni 9,174 zilizopangwa kutolewa.
Leseni hizo zilijumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, uchimbaji wa kati, uchimbaji mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini
Kati ya leseni zilizotolewa leseni 6,511 sawa na asilimia 70.97 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo, hii inadhihirisha azma ya serikali ya awamu ya 6 katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika sekta ya madini,"amesema.
Aidha amesema kuwa muelekeo wa sekta ya madini unalenga katika kuhakikisha mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika dira ya maendeleo ya Taifa, ilani ya chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango mkakati wa Tume ya madini wa mwaka 2019/20-2023/24.
Tume ya Madini ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya madini ambayo iliundwa na sheria ya madini sura ya 123 na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na.27, na ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi tarehe 17 aprili 2018.
Majukumu ya Tume ya madini yamefafanuliwa katika sheria ya madini sura ya 123 kifungu cha 22 ambayo yanalenga kusimamia shughuli zote zinazohusiana na madini nchini.
Lengo kuu la kuundwa kwa Tume ni kuboresha usimamizi na Udhibiti katika ukaguzi wa uzalishaji na biashara ya madini kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zote zinazoongoza shughuli za madini zinafuatwa ipasavyo ili kuongeza pato la Taifa.
0 Comments